Jumamosi , 21st Feb , 2015

Chama cha wananchi CUF visiwani Zanzibar kimezindua rasmi kamati za uchaguzi za chama hicho ambazo ni maalum kwa ajili ya kushughulikia masuala yote yanayohusu uchaguzi mkuu ujao ikiwa ni pamoja na maandalizi.

Akiongoza uzinduzi huo katika viwanja vya Mnazi mmoja leo mjini Zanzibar, katibu mkuu wa chama hicho Maalim Seif Shariff Hamad amesema kuwa huo ni miongoni mwa mikakati ya kuhakikisha chama cha CUF kinashinda uchaguzi ujao na kinaongoza Serikali ya Umoja wa kitaifa.

Amesema kupitia mikakati huo, viongozi wote wa chama hicho wamepewa vitendea kazi vya kutosha ikiwa ni pamoja na mashine za Photocopy na magari aina ya Vespar ili kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao bila malalamiko.

Maalif Seif amesema kuwa chama hicho ndicho kitakachoweza kuwakomboa wazanzibar na kuijenga Zanzibar huru yenye uwezo mkubwa wa kiuchumi itakayowahakikishia wazanzibari wote uhakika wa milo mitatu kwa siku.

“CUF haina tofauti na CCM, tena kwa hapa Zanzibar ni zaidi ya CCM kwahiyo tuhakikishe tunashinda kwa kura nyingi ili wasipate nafasi ya kuiba kura..”

Ameongeza kuwa kwa jinsi Zanzibar ilivyo,kijiografia ilipaswa kuwa kitovu cha biashara na uchumi kwa nchi za Afrika Mashariki na kati lakini inasikitisha kuona kuwa bado wananchi wake wanaishi katika maisha magumu na kiwango cha ukosefu wa ajira bado kiko juu.

Amehamasisha wanachama wenye uwezo hususani vijana wenye uwezo kujitokeza muda utakapofika kugombea nafasi mbalimbali

Pia Ametangaza rasmi kuunga mkono msimamo wa Umoja wa Katiba ya Wananchi wa kutoipigia kura Katiba Inayopendekezwa kwa madai kuwa haijakidhi madai ya wazanzibari.