Jumanne , 17th Mar , 2015

Bondia wa ngumi za kulipwa nchini Tanzania Francis Cheka aliyefungwa jela miaka mitatu kwa kosa la kushambulia na kudhuru mwili leo hii amebadilishiwa kifungo kutoka kifungo cha jela na kuwa kifungo cha nje.

Bondia huyo alifungwa jela Februari 3 mwaka huu na hakimu mkazi mwandamizi wa mahakama ya mkoa wa Morogoro Said Msuya kwa kosa la kumshambulia aliyekuwa meneja wa bar yake aitwaye Bahati Kibanda.

Akizungumza kutoka mjini Morogoro mwenyekiti wa huduma za jamii mkoani Morogoro (Parole) waliofanikisha zoezi hilo Yusuph Ponera amesema walifuatilia rekodi za bondia huyo kutoka mtaani kwake na kubaini kuwa hakuwa na rekodi yoyote ya makosa ya jinai na ndipo alipounganishwa katika idadi ya wafungwa waliohitaji kubadilishiwa kifungo.

Baada ya kusota gerezani kwa zaidi ya mwezi mmoja, akihukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela kwa shambulio la kudhuru mwili, hatimaye bondia wa dunia wa uzito wa kati (WBF) Francis Cheka amebadilishiwa adhabu na sasa atatumikia kifungo chake nje ya magereza.

Bingwa huyo mwenye rekodi ya kuwapiga wababe kibao wa ndani na nje ya nchi amefanikiwa kupata kifungo hicho  cha nje kutokana na kifungu cha sheria namba 3 ya Parole.

Katika kifungo chake cha nje cha miaka mitatu, cheka  atatakiwa kufanya kazi kwenye taasisi za umma ikiwemo ofisi ya mkuu wa mkoa, mkuu wa wilaya na taasisi zingine za umma.

Februari 02 mwaka huu, bondia Francis Cheka alihukumiwa  kifungo cha miaka mitatu jela na kutakiwa kulipa faini ya shilingi milioni moja mara atakapotoka gerezani na hakimu wa mahakama ya hakimu mkazi mkoa wa Morogoro Saidi Msuya kutokana na kutiwa hatiani kwa kosa la shambulio la kudhuru mwili dhidi ya meneja wa baa yake ya vijana Social, Rashid Kabanda.

Kwa mujibu wa mapromota wa ngumi Cheka anatarajiw kupanda ulingoni mwezi May mwaka huu kutetea ubingwa wake wa WBF uzani wa kati dhidi ya bondia atakayejulikana baadaye.