Jumatatu , 19th Jun , 2023

Mkurugenzi Mkuu Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Raymond Mndolwa amewataka wakulima wa Skimu ya Mahenge Wilayani Korogwe kulinda vifaa vya ujenzi  vitakavyotumika wakati wa Ujenzi na ukarabati wa Skimu hiyo ili kupata mradi wenye ubora na viwango stahiki. 

Akizungumza wakati wa hafla ya kumkabidhi eneo la mradi mkandarasi Gilco Construction Company Ltd, Mndolwa amesema wizi wa vifaa vya ujenzi unaweza kusababisha madhara makubwa ikiwemo kiwango kisicho sahihi.

Aidha Mndolwa amewaasa wananchi wa Korogwe kuwa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imeanza zoezi la Usanifu katika Bonde la mkomazi kwa gharama ya Tsh. Bilioni 22,  kwa lengo la kujenga Bwawa na skimu za umwagiliaji na kwamba zoezi la ujenzi wa Skimu litakapomalizika wenye mashamba makubwa watapunguziwa ili wananchi wengine wasio na mashamba wapewe.

 Kwa upande wake mkuu  wa Wilaya ya Korogwe mjini, Jokate Mwegelo amewataka wananchi wa Wilaya hiyo kuchangamkia fursa ya Kilimo cha Umwagiliaji ili kuinua maisha na pato la mtu mmojammoja na taifa kwa ujumla, huku akiwasisitiza waache tabia ya kuuza ama kukodisha mashamba yao.