Naibu Waziri wa Kazi na Ajira Mh. Dkt. Makongoro Mahanga
Akizungumza na HOTMIX Naibu Waziri wa Kazi na Ajira Mh. Dkt. Makongoro Mahanga amesema tatizo la ajira nchini ni kubwa lakini wizara yake imejipanga kukabiliana nalo kwa kutoa mafunzo na elimu ya ujasilia mali kwa vijana.
Aidha Mahanga ameitaka Serikali ijenge Viwanda ili vijana wengi wapate ajira pamoja na kujengwa kwa vyuo vya VETA, mpaka ngazi ya kata.
Mahanga amesema tatizo la Ajira kwa Tanzania japo halizidi asilimia 15 lakini vijana wengi hawana kazi za kufanya na kukimbilia kufanya uhalifu.
Wakati huo huo, Mpango wa kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge nchini Tanzania MKURABITA awamu ya Nne umewapa mafunzo wakulima 708 na viongozi wa Vyama vya Ushirika 141 kwa Manispaa 7 nchini ikiwa ni mpango wa kuwainua wananchi wanyonge kwa kurasimisha Ardhi na biashara zao hasa kwa maeneo ya vijijini.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Mratibu wa Mkurabita Bi. Saraphia Mgembe amesema pamoja na mafanikio hayo,bado kuna baadhi ya Halmashauri hushindwa kutenga fedha za kutosha kwa ajili ya mipango ya maendeleo.
Changamoto nyingine ni pamoja na wakulima wengi kukosa elimu ya kilimo cha kisasa na chenye tija pamoja na wingi wa Migogoro ya Ardhi pamoja na wakulima kushindwa kukopesheka na taasisi za kifedha kwa kushindwa kurasimisha Ardhi.