Ijumaa , 8th Sep , 2023

Salehe Rashid Lihanzi (47) mkazi wa Makangaga, Wilayani Kilwa Mkoani Lindi, amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Sokoine Mkoani humo baada ya watoto wake wa kambo kumshambulia kwa kumkata mapanga na kumpiga rungu kichwani, baada ya kuwataka warudishe kitanda walichouza bila makubaliano

Salehe amesema vijana wake walimwomba ruhusa ya kukaa kwenye nyumba yake wakati yeye na mama yao wakiishi shambani wakilinda na kulima Mahindi ambapo baada ya miezi mitatu kupita, alikwenda kijijini na kushangazwa na hali aliyoikuta kwani mlango wa nyumba ulikuwa umevunjwa, hakukuwa na pazia pamoja na kitanda.

"Nilishtushwa na mazingira niliyoyakuta kwasababu yule wa kiume mkubwa alikuwa ameshahama nyumbani, alichukua mapazia na kuyatumia kama mashuka huko kwa mwanamke alipohamia, kitanda hakikuwepo chumbani na mlango ulikuwa umevunjwa na kijana mdogo kwasababu kaka yake aliondoka na funguo na hiyo ikawa ndio njia yake ya kuingia ndani kulala" alisema Salehe Rashidi, majeruhi.

Baada ya kupigwa na Butwaa kwa hali aliyoikuta nyumbani, Salehe alimpigia kijana wake mkubwa aliyemtambulisha kwa jina la ALLY ALFANI na alipomuuliza vitu vimekwenda wapi alikana kufahamu na kumtaka baba yake wa kambo atulie ili yeye aendelee kufuatilia hivyo vitu.

Baada ya kupata majibu yasiyo mwingia kichwani aliamua kumsimulia mama mkwe (Mama wa Mwanamke anayeishi naye) naye alimjibu kuwa Huenda Mjukuuwe ameuza kwani alisikia tetesi za kijana huyo kuuza kitanda cha mama yake.

"Alivyoniambia kuwa alikuwa anauza kitanda cha mama yake nikajua ndio hiko hiko kitanda changu ...... Wakati narudi shambani nikakuta mwanamke wangu naye anakuja mjini nikamzuia kwakuwa kuna hatari ya wanyama, nikamsimulia kwamba kwa sasa hatuna kitanda watoto wameshauza....... na kwasababu anahusika na watoto wale nilimwomba awaulize wamekipeleka wapi? Aliyenunua arudishe na fidia atalipwa na aliyemuuzia kwasababu huo ni wizi"

Baada ya kumpatia taarifa hizo, mama huyo ambaye ameingia kwenye mahusiano na Salahe akiwa tayari ana jumla ya watoto sita "6" alijibu kuwa toka awali bwana Salehe hakuwa na mapenzi na watoto wake, huku akisema chuki yake ndio sababu ya kila kitu.

Anasimulia baadae wakati analinda shamba nyakati za saa saba mchana, aliwaona watoto 
wakimfuata shambani wakiwa wamegadhibika, yule mkubw akiwa ameshika upanga na rungu huku mdogo wake akiwa na upanga tu.

Anasema hakushtuka kwasababu ni watoto wake na anaamini wamemkosea hivyo alidhani wamedhamiria kumwomba msahama.

Baada ya kufika karibu yake walimshambulia kwa maneno wakimwambia yeye "anazingua" ambapo Salehe alionyesha msimamo wake na kuwaambia ni lazima warudishe kitanda ndipo Mtoto mkubwa alipomkata baba huyo upanga wa mguu na kumvunja mfupa wa mbele, mtoto mwingine akampiga upanga wa mguu wa pili ambao haukua na madhara makubwa na mwisho mtoto Mkubwa "Ally" alimpiga baba yake wa kambo Rungu la kichwa.

Kutokana na kushambuliwa kwake, anasema alipata msaada baada ya mama mkwe wake kwenda shambani kumwona kwani naye aliwaona wajukuze wakiwa na gadhabu. Kwa msaada wake na wananchi wengine alifanikuwa kufikishwa katika Zahanati kijijini hapo na baadae kusafirishwa hadi katika Hospitali ya Rufaa ya Sokoine mjini Lindi.

Jeshi la Polisi limethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo mpaka sasa wanaendelea kuwatafuta vijana hao wawili waliotoweka kusikojulikana baada ya kumshambulia kwa mapanga Baba yao wa Kambo.