Jumanne , 7th Nov , 2023

Wafanyabiashara wilayani Kisarawe mkoani Pwani, wameiomba Mamlaka ya Mapato (TRA) kuwapa elimu ya kutosha kuhusu ulipaji kodi wa hiari na matumizi ya mashine za EFD.

Ombi hilo limetolewa na baadhi ya wafanyabishara wilayani humo, wakati wa mkutano wao na viongozi wa Jumuiya ya Wafanyabishara (JWT) wakiongozwa na Mwenyekiti wake Hamis Livembe, wakiwa kwenye ziara ya kikazi ya kusikiliza kero mkoani humo.

Mfanyabishara Christina Mulu, amesema TRA wanatakiwa kuwapa elimu ya kutosha kuhusu ulipaji kodi badala ya kukazania kukusanya bila kuwasikiliza wafanyabishara kwanza.

“Wafanyabiashara wengi hatuna elimu ya kodi, matumizi ya EFD hatujui wakati mwingine risiti zinagoma kutoka na mashine kusumbua sasa TRA wakija wao ni kutaka tu kutoza faini badala ya kutupa elimu kwanza,” amesema Mulu.
Mfanyabishara John Masine, amewataka TRA kuwasaidia wafanyabishara urahisi wa kupata kodi na kuwalinda kwa kuondoa wamachinga mbele ya fremu za biashara.

“Mfanyabishara amekodi nyumba analipa kodi TRA, lakini anakuja mmachinga anaweka kibanda mbele yake na anauza bidhaa zinazofanana kwa bei ya chini zaidi na wala halipi kodi yoyote TRA zaidi ya ushuru wa serikali ya mtaa na hakuna anayejali zaidi ya kutaka kukamua kodi bila kujua tunauza au laa,” amesema Masine.

Naye Mfanyabishara Ester Moshi, ametaka wafanyabishara kutofunga biashara siku ya Jumamosi ya mwisho wa mwezi ambayo ni siku ya usafi kwasababu wanakwamisha shughuli za kiuchumi.

“Siyo kwamba siku hiyo biashara hazifanyiki hapana, zinafanyika lakini kwa kujificha na kukimbizana wakati serikali inaweza kupunguza muda ikawa muda wa kufungua ni saa 2 badala ya 4 asubuhi,” amesema Moshi.

Naye Ofisa wa TRA wilayani humo, Mohamed Chifu, ameushukuru uongozi wa JWT, kwa kazi kubwa wanayofanya ya kusikiliza kero za wafanyabishara lakini pia kutoa majibu ya kina kuhusu mambo mbalimbali yanayowahusu.
Amesema changamoto kubwa wanayokutana nayo TRA wilayani humo ni wafanyabishara wengi kuwa wa hali ya kati ambapo wanalipa kodi ndogo.

“Wengi wao wanalipa kodi ya ndogo kwa sababu ya halihalisi ya biashara, haujawa mji wa biashara kubwa. Kero ambazo zinatuhusu nimezibeba na naahidi nitaziwasilisha na kuzifanyia kazi,” amesema.