Jumanne , 26th Sep , 2023

Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Hassan Chande, amewataka Watanzania kuwa wazalendo zaidi katika kutoa na kudai risiti ya mashine za EFD ili kuhakikisha mapato ya nchi yanaongezeka na kusaidia kutekeleza miradi na huduma mbalimbali za kijamii.

Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Hassan Chande

Naibu Waziri Chande, ametoa rai hiyo wakati akizungumza na wafanyabiashara wa Kata ya Kiusa, wilaya ya Moshi Mjini, mKilimanjaro, akiwa katika ziara ya siku mbili mkoani humo iliyolenga kutatua changamoto mbalimbali wanazopitia wafanyabiashara mkoani humo na kuhamasisha matumizi sahihi ya mashine za kielektroniki (EFD).

"Lazima Watanzania tuwe na utamaduni wa kudai risiti tunaponunua bidhaa, na kutoa risiti tunapouza bidhaa, hii ndio chachu ya maendeleo ya nchi hii na itasaidia utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo maji, shule na afya ifanyike kwa wingi," amesema Mhe. Chande.

Aliongeza kuwa, kila Mtanzania anapaswa kuwajibika katika kulipa kodi na kudai risiti halali ya kieletroniki kila wanapofanya manunuzi na ameitaka Mamlaka ya Mapato (TRA), kuhakikisha wanakusanya mapato halali bila usumbufu kwa wafanyabiashara.