Monday , 26th Jan , 2015

Waziri wa mambo ya ndani ya Mathias Chikawe amelitaka Jeshi la Polisi kudhibiti wimbi la ongezeko wa uhalifu wa kimataifa ili lisiwe kuhatarisha amani ya nchi.

Waziri wa mambo ya ndani ya Mathias Chikawe

Chikawe ameonya kuongezeka kwa mitandao ya uhalifu wa kimataifa na ugaidi kama haitadhibitiwa mapema na vyombo vya ulinzi na usalama inaweza kujipenyeza katika sekta mbalimbali ikiwemo ya uongozi ili kujiwekea kinga na kujenga misingi ya kuendeleza uhalifu wao.

Amesema hali hiyo inaweza kuhatarisha utawala wa sheria, mfumo wa demokrasia na upatikanaji wa haki nchini.

Chikawe ameyasema hayo katika mkutano mkuu wa mwaka wa maafisa waandamizi wa jeshi la polisi nchini wenye lengo la kutathmini utendaji wa jeshi hilo kwa mwaka uliopita 2014 na mikakati ya mwaka 2015.

Waziri Chikawe anatumia nafasi hiyo kuwaonya maofisa hao kuwa macho na vitendo vya rushwa miongoni mwa watumishi wa vyombo vya usalama kutokana na uwezo mkubwa wa fedha chafu katika mitandao hiyo hasa wakati huu ambapo taifa linaelekea kwenye uchaguzi mkuu na upatikanaji wa katiba mpya.
 
Awali mkuu wa jeshi la polisi nchini IGP Ernest Mangu akizungumza katika mkutano huo, amesema kuwa pamoja na mambo mengine jeshi la polisi linakabiliwa na changamoto ya nidhamu katika utendaji wa jeshi hilo.

IGP Mangu pia amezungumzia mikakati ambayo inawekwa na jeshi hilo kwa kushirikiana na vyama vya siasa, msajili wa vyama na tume ya taifa ya uchaguzi ili kudhibiti matukio ya uvunjifu wa amani katika uchaguzi mkuu ujao na zoezi la upigaji kura ya maoni kwa ajili ya upatikanaji wa katiba.
 
Naye kaimu IGP Abdulrahmani Kaniki amewataka wananchi kuendelea kushirikiana na jeshi hilo kupitia falsafa yake ya polisi jamii na ulinzi shirikishi, ili kudhibiti matukio ya uhalifu.

Kaniki pia amejinadi kuwa jeshi hilo hivi sasa limeimarika katika idara zote ambapo mkuu wa mkoa wa Dodoma Chiku Galawa amelitaka jeshi hilo kutoa huduma bora kwa wananchi pasipo na kuhusishwa na vitendo vya rushwa ili kujenga imani ya jeshi hilo katika jamii. 
 
Mkutano huo wa siku 5 umebeba kauli mbiu isemayo NIDHAMU NI NGUZO THABITI KATIKA UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU YA JESHI LA POLISI.