Friday , 5th Jun , 2020

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli, amesema kuwa mara baada ya yeye kuingia madarakani walitokea watu na kumtuma Mgogo aje kuzusha kwamba, Tanzania ina ugonjwa wa Zika na ndipo alipoamua kumfukuza kazi kwa upotoshaji huo, kwa kuwa ugonjwa huo haujawahi kuwepo.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli.

Hayo ameyabainisha leo Juni 5, 2020, wakati akihutubia katika Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), uliofanyika jijini Dodoma, na kuongeza kuwa mpaka sasa ni karibu miaka mitano tangu achukue uamuzi huo, lakini hajawahi kusikia kesi za ugonjwa huo.

"Kwa nchi yoyote inayojitegemea inatengeneza maadui na ndiyo maana wakati tunaingia madarakani tuliambiwa Tanzania tuna ugonjwa wa Zika, aliyetangaza na aliyetumiwa kutangaza nikamfukuza kazi bahati mbaya ni Mgogo, baada ya kumfukuza waliomtuma wakampa Ukurugenzi, kuanzia tulipomtoa ni miaka karibu mitano hapajawahi kuwa na kesi ya Zika hapa, baadaye likazushwa na kuambiwa tuna Ebola" amesema Rais Magufuli.

Ikumbukwe kuwa Disemba 16, 2016, Rais Dkt Magufuli, alitengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Dkt Mwele Malecela.