Dk. Phillip Mpango
Akizungumza katika Ofisi za Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Mpango amezishukuru taasisi, mashirika ya umma na vyuo vikuu hivyo kwa kufanikisha kutoa michango ambayo itasaidia kuboresha maisha ya watanzania.
Aidha Waziri Mpango amewasisitiza wenyeviti na wakurugenzi watendaji wa taasisi na mashirika ya umma ambao hayajatoa gawio na michango ya serikali hadi kufikia Januari 23 saa sita usiku kujiondoa katika nafasi zao na wasisubiri barua.
Amesema kuwa ni vema kuhakikisha watu waliopewa dhamana katika Taasisi na Mashirika ya Umma wanatumia rasilimali zilizopo katika kuiwezesha Serikali kujitegemea kuliko kutegemea wafadhili ambao kwa sasa wanapeleka nguvu kubwa katika nchi zao.
“Nawahakikishia kuwa fedha hizi zilizopokelewa katika Mfuko Mkuu wa Hazina zitatumika kwa ajili ya kuboresha maisha ya wananchi masikini kwa kuwa taasisi za umma zilianzishwa ili uwekezaji wake uwanufaishe wananchi na Taifa kwa ujumla”, alieleza Dkt. Mpango.
Miongoni mwa Taasisi zilizowasilisha gawio na michango ni pamoja na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Chuo cha Ushirika Moshi, Chuo Kikuu cha Mzumbe, Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), Star Media, Bodi ya Utalii, Shirika la Maendeleo la Taifa na Bodi ya Wataalamu wa Manunuzi na Ugavi (PSPTB).
Zaidi ya Sh. trillion 1.2 zimekusanywa kutoka katika Taasisi, Kampuni na Mashirika ya Umma 230 ikiwa ni gawio na michango mbalimbali kuanzia Novemba 24 mwaka jana hadi Januari 7, mwaka huu.

