Friday , 6th Sep , 2019

Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto  Ummy Mwalimu, amewataka watanzania kuhakikisha wanajiunga na Mfuko wa Bima ya afya ili kupunguza gharama za matibabu, pindi wanapopatwa na matatizo badala ya kutumia fedha hizo katika masuala yasiyokuwa na tija.

Waziri Ummy Mwalimu

Waziri Ummy ameyasema hayo leo Septemba 06, katika mkutano wa 16 wa Bunge la 11, wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu Faida Bakari, lililohoji juu ya zuio la kuchukua maiti,  linalofanywa na Serikali baada ya ndugu kushindwa kulipa gharama za kuchukua mwili na ndipo alipotoa mfano wa Mwanamke aliyefanya sherehe na matarumbeta mara baada ya mume wake kuachana na mchepuko.

''Mheshimiwa Mwenyekiti nataka kutoa mfano hapa,  wote tumeona kwenye mitandao Mama anashangilia Mume amerudi nyumbani kwa sababu ametoka kwa nyumba ndogo, matarumbeta ni Shilingi ngapi ambayo amekodi, wamenunua sare, wameweka mishikaki gharama pale ni kama laki 3, Toto afya kadi ni 50400, halafu leo mtu analalamika sina fedha nisaidiwe, kama kweli tunataka kupata huduma nzuri wananchi tuwe tayari kujiunga na mifuko ya bima ya afya'', amesema Waziri Ummy.

Waziri Ummy akifafanua zaidi kuhusu suala la miili kulipiwa gharama amesema kuwa, Serikali haidai gharama za kumlipia maiti, bali gharama inayodaiwa ni ile inayotumika wakati akipatiwa huduma kabla ya mauti kumfika.