Kikosi cha mabingwa wa ligi kuu Tanzania bara timu ya Yanga.
Michezo ya mwisho ya Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara, inatarajiwa kufanyika leo Jumapili, Mei 22, 2016 kwa timu zote 16 kutinga katika viwanja vinane tofauti kumaliza ngwe ya msimu wa 2015/16.
Michezo itakayopigwa kesho ni pamoja na Simba itakayokipiga na JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wakati Azam FC ambayo inawania nafasi ya pili kama Simba, itakipiga na African Sports kwenye Uwanja wa Azam Complex, ulioko Chamazi, Mbagala nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.
Mabingwa wa Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara, Yanga ya Dar es Salaam inakaribishwa na wanalizombe Majimaji ya Songea kwenye Uwanja wa Majimaji mjini humo ilihali Mwadui na Kagera Sugar nazo zitamaliza ligi katika Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.
Kadhalika kwa mujibu wa ratiba hiyo ya Ligi Kuu ya bara, Toto Africans itakuwa mwenyeji kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza kuikaribisha Stand United, wakati African Sports ‘Wanakimanumanu’ wameifuata Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Manungu, Mvomero mkoani Morogoro.
Mechi nyingine ya kukunja jamvi kwenye Ligi Kuu VPL zitakuwa kati ya Mbeya City dhidi ya Ndanda FC ya Mtwara huku mchezo mwingine wenye presha utakuwa ni kwa Tanzania Prisons yenye pointi 48 ambayo licha ya kucheza na Coastal Union ambayo tayari imeshuka daraja kwenye Uwanja wa Mkwakwani, itakuwa inafukuziwa na Mtibwa Sugar kuwa na nafasi ya nne. Mtibwa Sugar ina pointi 47 na mvutano ni wa nafasi ya nne hasa ukirejea kwenye zawadi.
Presha kubwa ni kwa Simba na Azam ambazo zina tofauti ya pointi moja katika msimamo wa ligi hiyo iliyoshirikisha timu 16. Azam FC ina pointi 63 ikishika nafasi ya pili nyuma ya mabingwa Yanga huku Simba inayoshika nafasi ya tatu ina pointi 62.
Yanga ambayo imetwaa ubingwa, tayari imepewa taji na medali kwa wachezaji 24, viongozi saba wa benchi la ufundi na viongozi wanne wa Kamati ya Utendaji Jumamosi iliyopita na inachosubiri ni fedha kiasi cha Sh 81,345,723 wakati Azam na Simba zinawania zawadi ya mshindi wa Pili Sh 40,672,861 na Mshindi wa Tatu Sh 29,052,044 huku Prisons na Mtibwa Sugar zikichuana kupata zawadi ya Mshindi wa Nne ambayo ni Sh 23,241,635.
Pia timu zote zinawania zawadi ya Mchezaji Bora ambayo ni Sh 5,742,940 kiwango kinachofanana na atakachopewa Mfungaji Bora wa Ligi na Kipa Bora wa michuano hiyo inayodhaminiwa na Vodacom wakati Mwamuzi Bora atazawadiwa Sh 8,614,610 kiwango kinachofanana atakachopewa Kocha Bora wakati timu yenye nidhamu itavuna Sh 17,228,820.
Tayari Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limetoa onyo kwa timu zote kutojiingiza kwenye mtego wa aina yoyote wa kupanga matokeo na kwamba michezo yote haina budi kuanza saa 10.00 jioni hata kama kutakuwa na hali ya mvua katika viwanja husika lengo likiwa ni kukabiliana na upangaji wa matokeo.
Baada ya michezo 29 kwa kila timu, tayari Coastal Union ya Tanga ikiwa imeaga rasmi Ligi hiyo na kwamba kuna timu tano ambazo baadhi yake (timu mbili) zikipata matokeo mabaya zitaungana na Wagosi wa Kaya kushuka daraja msimu wa 2015/16. Coastal Union yenye pointi 22 na hata ikishinda mchezo wa mwisho, haiwezi kuzifikia timu zilizo juu yake.
Timu ambazo ziko kwenye hatari ya kushuka ni African Sports ya Tanga yenye pointi 26 (nafasi ya 15); Mgambo pia ya Tanga iliyojikusanyia pointi 27 (nafasi ya 14); Kagera Sugar ya Kagera iliyovuna pointi 28 (nafasi ya 13); JKT Ruvu ya Pwani iliyopata pointi 29 (nafasi ya 12) na Toto Africans ya Mwanza yenye pointi 30 (nafasi ya 11).
Kwa hali ya mambo ilivyo, licha ya kwamba Toto inaweza kujihesabu ina nafuu ikilinganishwa na timu nyingine, ukweli unabaki kuwa kwa timu zenye pointi 27 hadi 29 zinaweza kuishusha kama Wanakishamapanda hao watapoteza mchezo wa mwisho au kupata sare huku wapinzani wao wakishinda.