Kikosi cha timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 17 Serengeti Boys.
Timu ya Taifa ya Vijana wenye umri chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) inatarajiwa kucheza michezo miwili ya kirafiki na timu ya Taifa ya Misri Vijana wenye umri chini ya miaka 17 (The Pharaohs) jijini Dar es salaam.
Mchezo wa kwanza kati ya Serengeti Boys dhidi ya The Pharaohs utachezwa siku ya Jumamosi, Aprili 2 katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam, huku mchezo wa pili ukichezwa Jumanne Aprili 5 katika uwanja wa Azam Complex Chamazi.
Msafara wa The Pharaohs unatarajiwa kuwasili Alhamis tarehe 31, Machi ukiwa na watu 33, wakiwemo wachezaji 25 pamoja na viongozi 8, na wataondoka nchini tarehe 6 Aprili kurudi kwao nchini Misri.
Kikosi cha Serengeti Boys kinachonolewa na makocha Bakari Shime na Sebastian Mkomwa wakishauriwa na Kim Poulsen, kimeendelea na mazoezi katika uwanja wa Karume, zilipo ofisi za Makao za Makuu ya TFF.
Serengeti Boys ilingia kambini takribani wiki mbili zilizopita katika hosteli za TFF zilizopo Karume, kujiandaa na michezo hiyo miwili ya kirafiki ya kujipima nguvu kujiandaa kuwania kufuzu kwa Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Vijana wenye umri chini ya miaka 17 zitakazofanyika mwaka 2017 nchini Madagascar.
Tanzania itaanza kuwania kufuzu kwa fainali hizo mwishoni mwa mwezi Juni, kwa kucheza dhidi ya timu ya Taifa ya Vijana ya Shelisheli.
Wakati huo huo Kombe la Shirikisho (Federation Cup) linatarajiwa kuendelea Alhamisi kwa michezo miwili kuchezwa katika hatua ya robo fainali ya michuano hiyo.
Azam FC watakua kwenye uwanja wa Azam Complex kuwakaribisha maafande wa Tanzania Prisons kutoka jijini Mbeya siku ya Alhamis saa 10 jioni kwa saa za Afrika Mashariki.
Young Africans watakua wenyeji wa Ndanda FC kutoka Mtwara katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam, huku kila timu ikihitaji ushindi katika michezo hiyo ili kuweza kufuzu kwa hatua ya nusu fainali.
Aprili 11, Simba SC watakamilisha hatua ya robo kwa fainali kwa kucheza na wagosi wa kaya Coastal Union katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Mwadui FC ndio timu pekee mpaka sasa ambayo imeshafuzu kwa hatua ya nusu fainali, baada ya kuwachapa Geita Gold kwa mabao 3 -0.
Bingwa wa michuano ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) atawakilisha Tanzania mwakani kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika (CAF CC) mwaka 2017.