Saturday , 6th Feb , 2016

Ligi kuu ya soka Tanzania bara VPL inataraji kuendelea Jumapili hii kwa mzunguko wa 18 kwa viwanja saba kuwaka moto kwa timu 14 kusaka alama tatu muhimu ili kujiimarisha katika msimamo wa ligi hiyo yenye timu 16.

Ligi hiyo ambayo hivi sasa imefikia patamu hasa kutokana na timu tatu za juu Yanga, Simba na Azam kufukuzana kwa alama sawa kwa Simba na Azam zenye alama 39 kila moja huku kinara Yanga ambao ndiyo mabingwa watetezi wakiongoza kwa tofauti ya alama moja kwakuwa na alama 40 kitu ambacho kinaongeza ushindani na kufanya ligi hiyo kuwa na ugumu wa aina yake hasa katika kipindi hiki ambacho inaelekea katika hatua za lala salama.

Michezo saba itakayochezwa siku ya Jumapili ni pamoja na mchezo wa maafande wa JKT Ruvu ambao wao watakuwa wenyeji wa Young Africans katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam, Nao wagonga nyundo wa jiji la Mbeya, Mbeya City watacheza dhidi ya Tanzania Prisons uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, huku wana kuchele timu ya Ndanda FC wao watawakaribisha Mtibwa Sugar katika uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.

Katika Shinyanga wenyeji Kagera Sugar watacheza dhidi ya Simba SC katika uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, wakati wana rambaramba Azam FC watawakaribisha wachimba migodi toka Shinyanga Mwadui FC uwanja wa Azam Complex Chamazi, huko Ruvuma wenyeji wana lizombe timu ya Majimaji wao watakuwa na kibarua dhidi ya maafande wa JKT Mgambo kwenye uwanja wa Majimaji mjini Songea na jijini Mwanza wana kishamapanda Toto Africans watawakaribisha wagosi wa kaya Coastal Union katika uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.