Mshambuliaji wa Simba Ibrahim Ajib akikabidhiwa mpira katika moja ya michezo aliyopiga magoli matatu 'hat-trick'
Kamati ya usajili ya klabu ya soka ya Simba imesema imeshitukia mchezo mchafu unaotaka kufanyika juu ya usajili wa mshambuliaji kinda wa timu hiyo Ibrahim Ajib Migomba ambaye ametimkia nchini Afrika Kusini bila ruhusa ya uongozi wa timu hiyo.
Ajib aliondoka nchini asubuhi ya jumatatu, ikiwa ni siku moja tangu atolewe kwa kadi nyekundu katika mchezo wa Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara timu yake, Simba ikilala 1-0 mbele ya Mwadui FC ya Shinyanga Uwanja wa Taifa, Jumapili.
Na kwa sababu kwa kadi Ajib asingeweza kucheza mechi mbili kati ya tatu za mwisho za Simba, akaona ni wakati mwafaka kutimiza mpango wake wa kwenda kujaribu bahati yake sehemu nyingine.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya klabu hiyo Zacharia Hans Poppe amesema kuna timu inataka kufanya mchezo mchafu kwakushirikiana na shirikisho la Soka nchini TFF kama ilivyokuwa katika usajili wa kina Singano na Mbuyu Twite.
Aidha, Poppe ambaye amekuwa kama muhimili wa klabu hiyo katika masuala ya kifedha amekiri kutofahamu lolote juu ya majaribio ya kinda huyo nchini Afrika Kusini lakini pia hata taarifa za safari yake nchini huo kitu ambacho kinawatia shaka viongozi wa timu hiyo na kuamua kuweka wazi juu ya mchezo huo anaouita ni mchafu kuchezwa na vilabu vyenye fedha nchini [Yanga na Azam] ambavyo kwa nyakati tofauti wamekuwa wakifanya usajili wa wachezaji wa Simba kinyume na kanuni ama taratibu za mpira na wakafanikiwa kuwatumia wachezaji hao kupitia mgongo wa Shirikisho la Soka nchini TFF.
Poppe amesema ni ngumu kwa mpira wa nchi hii kuendelea kwa mtindo wa aina hii wakupindisha sheria na ukiukwaji wa wazi kwa makusudi wa kanuni za soka kama unavyofanywa na vilabu vyenye pesa vikishirikiana na baadhi ya watu waliokatika kamati mbalimbali za maamuzi ndani ya Shirikisho la Soka nchini TFF.
Poppe amesema walishapoteza haki yao zaidi ya mara tatu katika usajili wa wachezaji ambao walikuwa na mikataba nao kisha kwa hila za vilabu vya Yanga ambao waliwapoka Mrisho Ngasa, Mbuyu Twite na Kelvin Yondan na Azam fc waliowapoka Ramadhan Singano 'Messi' kwa kushirikiana na TFF, safari hii wameona mchezo huo huo unaweza kutoke pia kwa Ajib ambaye alisaini mkataba wa miaka mitatu na timu hiyo ambao mpaka sasa umebakiza msimu mmoja [mwaka].
Akimalizia Poppe ameitaka taasisi ya kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini TAKUKURU kuingilia kati masuala ya michezo ambayo yanaonyesha wazi kunaviashiria vya mchezo mchafu [rushwa] ambayo ni moja ya changamoto kubwa katika sekta ya michezo nchini na duniani kote huku akitolea mfano mchezo baina ya wenyeji Ndanda FC ya Mtwara dhidi ya Yanga uliokuwa ufanyike Mtwara eti umehamishiwa jijini Dar es Salaam baada ya kufanyika makubaliano baina ya pande zote mbili.
Poppe amesema chakushangaza ni makubaliano hayo kufanyika kinyume na taratibu za soka akimaanisha sheria, kanuni na ataratibu stahiki za kimpira na pia baya zaidi akidai kitendo cha Yanga kuwagharimia kila kitu wapinzania wao hao kitu ambacho Poppe amesema ni wazi kinatengeneza mazingira ya kutokuwa na ushindani jambo ambalo kwa tafsiri ni rushwa ya upangaji matokeo hivyo TAKUKURU ameiomba taasisi hiyo igekukie na upande huo ambao ameuita ni jipu.