Sunday , 1st May , 2016

Unaweza kusema kuwa matokeo ya suluhu ya timu za Simba na Azam katika mchezo wa hii leo ni kama wameisafishia njia timu ya Yanga amabao ndiyo mabingwa watetezi wa ligi hiyo na sasa inajidai kileleni ikiziacha timu hizo kwa alama saba katika msimamo.

Viungo wa timu za Simba na Azam Jonas Mkude 'fundi' [kulia] na Salum Aboubakar 'sure boy' wa Azam [kushoto] wakiwania mpira.

Klabu za soka za Simba SC na Azam FC zimetoshana nguvu kwa kwenda suluhu ama sare ya bila kufungana katika mchezo wa Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara uliofanyika jioni ya leo katika uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Matokeo hayo yamepokewa kwa furaha na mahasimu wao Yanga ambao sasa wanaongoza Ligi Kuu hiyo kwa wastani wa pointi sita kuelekea mechi nne za mwisho.

Kwa sare hiyo ya 0-0, Azam FC inafikisha pointi 59, wakati Simba sasa inakuwa na pointi 58, nyuma ya mabingwa watetezi, Yanga wenye pointi 65 baada ya timu zote kucheza mechi 26.

Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Mathew Akrama kutoka jijini Mwanza, aliyesaidiwa na washika vibendera Abdallah Mrisho wa Pwani na Omar Kambangwa wa Dar es Salaam hakukuwa na mashambulizi ya kusisimua na timu zote zilionekana kucheza kwa tahadhari kupita kiasi, hivyo kuufanya mchezo upooze hasa katika kipindi cha kwanza japo kulikuwa na kosakosa za hapa na pale kwa pande zote mbili.

Kipindi cha pili, kilianza kwa mchezo wa kukamiana na kuchezea rafu na undava, jambo ambalo hata hivyo refa Akrama alilidhibiti kwa busara za kuwatuliza wachezaji wa timu zote mbili kwa kuzungumza nao mara kwa mara na kufanya hali ya hewa kurejea tena kama kawaida.

Baada ya hapo, kidogo mchezo wenye hadhi ya timu kubwa katika Ligi Kuu ya nchi, tena zinazowania ubingwa ndiyo ukaanza kuonekana kwa mshambulizi ya pande zote mbili kwa nyakati tofauti.

Nahodha wa Azam FC, John Bocco peke yake akakosa mabao mawili ya wazi na kushika kichwa kwa masikitiko, wakati upande wa Simba Hamisi Kiiza na Hajji Ugando walipoteza pia nafasi za wazi.

Kwa hali ilivyosasa vilabu hivyo vikubwa vitatu ambavyo vyote vimebakiwa na michezo minne kuhitimisha ligi hiyo kila mmoja atakuwa akimwombea njaa mwenzake apoteze michezo yake ama kutoka sare huku yeye akiibuka na ushindi jambo ambalo ni sawa na fisi kuomba mkono wa binadamu udondoke wakati akitembea.

Lakini pamoja na hilo kwa timu hizo zote tatu Simba na Azam pamoja kuwa nyuma kwa alama zaidi ya sita lakini unafuu wa timu hizo unatokana na ratiba kwakuwa kati ya michezo minne iliyobaki kwao miwili watacheza nyumbani na miwili ugenini huku kwa upande wa vinara Yanga wao michezo yao yote minne wanapiga ugenini.