Wednesday , 23rd Mar , 2016

Pamoja na malalamiko kibao kutoka kwa baadhi ya vilabu kuwa ratiba ya ligi kuu ya soka Tanzania bara VPL inavibana baadhi ya vilabu na kuvipa unafuu baadhi ya vilabu lakini kwa hali ilivyo bodi ya ligi imetamka kuwa panguapangua ya ratiba haiepukiki.

Wachezaji wa timu za Yanga na Azam wakichuana katika moja ya michezo iliyozihusisha timu hizo.

Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi , Boniface Wambura amesema kwamba wamelazimika kupangua Ratiba ya Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara, iwapo Azam fc na Yanga sc zitasonga mbele kwenye michuano ya vilabu barani Afrika.

Azam fc wao watamenyana na Esperance ya Tunisia katika Raundi ya Pili ya michuano ya Kombe la Shirikisho na wakifanikiwa kuitoa timu hiyo, watakwenda kwenye mchujo wa kuwania kucheza hatua ya makundi ya michuano hiyo.

Kwa upande wa Yanga wao watamenyana na Al Ahly ya Misri katika hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika na wakiitoa watakwenda hatua ya makundi wakati wakitolewa watahamia kwenye mchujo wa kuwania tiketi ya makundi ya kombe la Shirikisho.

Na kwa sababu hiyo, Wambura amesema; “Iwapo Azam itasonga mbele itacheza mechi hizo za mtoano, wakati Yanga yenyewe itacheza tu mechi hizo za mtoano iwapo itatolewa katika raundi inayofuata ya Ligi ya Mabingwa,”.

“Hivi sasa Azam na Yanga zinashiriki hatua ya 16 bora ambayo itachezwa kati ya Aprili 8-10 kwa mechi za nyumbani, na Aprili 19 na 20 kwa mechi za ugenini,”.

“Mechi za kwanza za raundi ya mtoano (play offs) zitachezwa kati ya Mei 6-8 wakati za marudiano zitafanyika Mei 17-18. Yanga ikiitoa Al Ahly maana yake haitacheza hatua ya mtoano (play offs), na badala yake itasubiri moja kwa moja hatua ya makundi ambayo mechi zake za kwanza zitafanyika kati ya Juni 17-19,”.

“Marekebisho mengine yanaweza kufanyika kwa kuzingatia matokeo ya scenario hizo hapo juu,”.