Thursday , 5th Nov , 2015

Wanafunzi wa shule ya msingi Nanyati, kata ya Mkunwa katika halmashauri ya Mtwara vijijini wanalazimika kusomea chini ya miti na wengine kukaa chini kutokana na kukosa madarasa na madawati, baada ya shule hiyo kuwa na chumba kimoja.

Baadhi ya wanafunzi wakionekana wakisomea chini ya mti (Picha na maktaba Yetu).

Wakizungumza shuleni hapo, wanafunzi hao wameitaka serikali kuwatatulia changamoto hizo ambazo wamezitaja kuwa ni kikwazo katika safari yao ya kujipatia elimu kutokana na muda mwingi kukosa masomo zaidi inaponyesha mvua.

Naye, mwalimu mkuu wa shule hiyo, Shaibu Hoja, amezitaja changamoto nyingine, kuwa ni kukosa vyoo, nyumba za walimu, ofisi za walimu pamoja na ukosefu wa madawati ambapo yaliyopo ni madawati 26 huku shule ikihitaji madawati 88.

Kwa upande wake, kaimu mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Tamimu Kambona, ambaye pia ni afisa elimu shule za msingi, amesema wanazo taarifa juu ya shule hiyo na kwamba tatizo lililokwamisha ujenzi wa madarasa ni kutokana na kuwekeza nguvu nyingi katika ujenzi wa maabara ambao uligharimu pesa nyingi.