Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora nchini kupitia Mwenyekiti wake Bw. Bahame Nyanduga imebaini ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu katika tukio la jeshi la polisi la kuwapiga na kuwadhalilisha viongozi na wafuasi wa chama cha CUF eneo la Mtoni Mtongani wilaya ya Temeke Jijini Dar es Salaam, Januari 27 mwaka huu.
Tume imebaini kuwa jeshi la polisi nchini lilitumia nguvu nyingi kupita kiasi na kusababisha majeraha kwa viongozi wa chama hicho na wakazi kwa maeneo hayo kwa kutumia mabomu ya machozi hata pale ambapo haikuhitajika kufanya hivyo, pamoja na kuwadhalilisha kijinsia wanachama wawili wanawake wa CUF.
Aidha tume hiyo kwa kupitia Mwenyekiti wake Bwana Nyanduga imelitaka jeshi la Polisi lizingatie kanuni,sheria, haki za binadamu na misingi ya utawala bora katika utekelezaji wa majukumu yake na litoe mafunzo kwa maafisa na askari watakaoratibu na kushughulikia masuala yote yatakayojitokeza.