Zaidi Ya Watu 8,000 wanakadiriwa kuwasili nchini Burudi siku mbili zilizopita, huku watu 30,000 wakiwasili ndani ya wiki moja wakati waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda na jeshi lake wakiingia jana Jumanne katika mji wa kimkakati wa Uvira ulio karibu na mpaka na nchi jirani ya Burundi mashariki mwa DRC.
Wapiganaji kutoka kundi hilo lenye silaha linaloipinga serikali wameingia katika mji huo wenye wakazi laki kadhaa kutoka kaskazini, katika vurugu mpya ambazo zimekuja siku chache tu baada ya kuidhinishwa, chini ya usimamizi wa Washington, kwa makubaliano ya Kinshasa-Kigali yenye lengo la kurejesha amani mashariki mwa Kongo, eneo linalopakana na Rwanda na lenye rasilimali nyingi, lakini linalokumbwa na migogoro kwa takribani miaka thelathini.
Mpango huu mpya wa kundi lenye silaha la M23 na washirika wake wa Rwanda linaloipinga serikali unakuja karibu mwaka mmoja baada ya shambulio kubwa lililowawezesha, kati ya mwezi Januari na Februari, kuteka miji miwili mikubwa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Goma na Bukavu.
Mapema Alhamisi ya wiki iliyopita, Rais wa Kongo Félix Tshisekedi na mwenzake wa Rwanda, Paul Kagame, waliidhinisha makubaliano huko Washington yenye lengo la kukomesha mgogoro huo, ambao Rais wa Marekani Donald Trump aliusifu kama "muujiza."
Makubaliano hayo yanajumuisha sehemu ya kiuchumi inayoahidi kuhakikisha usambazaji wa madini ya kimkakati kwa ajili ya sekta iliyoendelea ya Marekani.
Mapema jana wakazi katika jiji hilo, lililoko kati ya milima na Ziwa Tanganyika, walikuwa wakitoroka makazi yao, huku wakazi, wanajeshi, maafisa wa polisi, na wafanyakazi wa utawala wakikimbia tishio hilo.





