Jumanne , 15th Apr , 2025

Michezo ya robo fainali mkondo wa pili ya Ligi ya mabingwa barani Ulaya kuendelea hii leo Jumanne kwa michezo miwili kupigwa. Kikosi cha Aston Villa kitawakaribisha PSG katika Uwanja wa Villa park majira ya Saa nne usiku huko nchini England.

Michezo ya marudiano ya UEFA CL leo

Villa walipoteza mchezo wa mkondo wa kwanza kwa idadi ya magoli 3-1. kikosi hicho cha Kocha Unai Emery kinahitaji kushinda mchezo huo kwa idadi ya kuanzia magoli 3-0 ili kuvuka na kutinga hatua ya nusu fainali, huku PSG wao wanahitaji sare au ushindi wowote kufuzu hatua hiyo. 

 Mchezo mwingine utapigwa pale Uwanja wa Signal Iduna Park nchini Ujerumani, ambapo kikosi cha Borussia Dortmund kitawakaribisha FC Barcelona majira ya Saa nne usiku. BVB walipoteza mchezo wa kwanza huko Catalonia nchini Hispania kwa idadi ya magoli 4-0, kikosi hicho kinapaswa kushinda mchezo wa leo kuanzia idadi ya magoli 5-0 ili kuvuka hatua hii huku Barcelona wanahitaji hata sare kutinga hatua ya nusu fainali kwa mara ya kwanza tangu 2018/19.

Katika hatua nyingine kikosi cha Real Madrid hapo kesho Jumatano kitakuwa mwenyeji wa Arsenal huko nchini Uhispania. Los Blancos wanapaswa kupindua matokeo 3-0 dhidi ya washika mitutu hao wa London, mchezo walioupoteza Juma lililopita nchini England   ili kufuzu hatua ya nusu fainali huku kikosi cha Inter Milan kutoka nchini Italia kitakuwa na kazi ya kulinda ushindi walioupata katika mchezo wa mkondo wa kwanza wa magoli 2-1 nchini Ujerumani dhidi Bayern Munich.