Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam SACP Jumanne Muliro, na kulia ni Daisle Simion Ulomi
Taarifa hiyo imetolewa leo Desemba 16, 2024 na Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo SACP Jumanne Muliro ambapo ameeleza kuwa tarehe 11 Desemba, 2024 Jeshi hilo lilipata taarifa ya kupotea kwake na ndugu hawakuwa wanampata kwenye mawasiliano ya simu, baada ya yeye kuondoka ofisini kwake Sinza na kudai anaelekea Temeke kufuatilia makontena yake ya biashara.
"Ulomi aliondoka eneo lake huku akitumia pikipiki namba MC 415 DQC aliyokuwa akiendesha mwenyewe, ufuatiliaji umefanyika kwa kushirikiana na ndugu na kubainika kuwa Ulomi alipelekwa kituo cha afya cha Makuburi Ubungo External mchana wa tarehe 11 Desemba, 2024 baada ya kupata ajali mbaya na pikipiki aliyokuwa akiitumia, wasamaria wema walimsadia kumpeleka kwenye kituo hicho akiwa hajitambui na hakuwa na kitambulisho chochote," imeeleza taarifa ya Kamanda Muliro.
Aidha taarifa hiyo imeeleza kuwa, " Baadae alipelekwa Mwananyamala hospitali na ikabainika tayari alikuwa amefariki na maiti yake kuhifadhiwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali hiyo kama mtu asiyefahamika akisubiri kutambuliwa na ndugu, ndugu tayari wameutambua mwili huo ukiwa na majeraha maeneo mbalimbali ya mwili. Aidha, Pikipiki aliyopata nayo ajali pia imepatikana ikiwa imeharibika. uchunguzi zaidi wa ajali hiyo unaendelea na taarifa zaidi itatolewa,".