Jumatano , 7th Aug , 2024

Makocha wa Simba na Yanga wameeleza mipango yao kuelekea mchezo wa nusu fainali ya ngao ya jamii ambao utazikutanisha timu hizo za kariakoo hapo kesho. Kocha wa Simba Fadliu Davis atakuwa akicheza mchezo wake wa kwanza wa dabi ya Kariakoo na ameweka wazi kuwa hautakuwa mchezo mwepesi.

Kocha mkuu wa Simba SC Fadlu Davis amekiri kuwa hautokuwa mchezo mwepesi kwao ukizingatia timu yake imepata wiki 4 tu za maandalizi na kikosi chake kinaundwa na nyota wengi wapya waliojiunga na timu hiyo msimu huu.

“Sio mechi yenye tofauti kubwa kwa ubora wa wachezaji, tofauti ni kwamba wenzetu yanga wachezaji wao wamecheza kwa pamoja kipindi kirefu, jambo linalo rahisisha mawasiliano yao wakiwa uwanjani, Ila tuna timu mpya na nzuri ambayo tunajua namna gani ya kuwakabili wapinzani, Sio rahisi kutabiri kikosi chetu wala aina ya mfumo tunaobtumia, huwa tunabadilika kutokana na mahitaji ya mchezo.” amesema   Fadlu.

Miguel Gamondi kocha wa Yanga amesema ataingia kwa kuwaheshimu wapinzani wao Simba kwenye mchezo huu wa kesho.

“Mara zote nawaheshimu wapinzani wangu, ina kocha na wachezaji wapya ambao wanataka kuonesha uwezo wao, sito wachukulia simba kama timu nyepesi, tuna uteyari wa kupambana kuhakikisha tunashinda bila kumdharau mpinzani na kutumia nafasi tunazo zitengeneza kwa umakini.” Amesema  Gamondi.
 

Mchezo huu wa kariakoo dabi utachezwa Saa 1 kamili usiku uwanja wa benjamini mkapa Dar es salaam na huu ni mchezo wa nusu fainali ya pili ya michezo ya ngao ya Jamii. Mshindi wa mchezo huu atakutana na mshindi wa mchezo wa nusu fainali ya kwanza inayozikutanisha Coastal Union na Azam FC.