Jumatano , 28th Feb , 2024

Tanzania inatazamiwa kuwa sehemu ya soko la umeme pale nchi jirani zitakapohitaji nishati hiyo, na hii ni baada ya kuwashwa kwa mashine zote Tisa katika Bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere ambalo litazalisha megawati 2,115 ambazo zinatoa uhakika wa kutosheleza mahitaji ya ndani.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko akizungumza katika mkuwatano wa 18 wa Baraza la Mawaziri wanaohusika na mfumo wa pamoja wa umeme kwa nchi za Mashariki mwa Afrika (EAPP Council of Ministers-COM) ambao unafanyika kwa siku mbili jijini Nairobi nchini Kenya.

Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko Februari 27, 2024 katika Mkutano wa 18 wa Baraza la Mawaziri wanaohusika na mfumo wa pamoja wa umeme kwa nchi za Mashariki mwa Afrika (EAPP Council of  Ministers-COM) ambao unafanyika kwa siku mbili jijini Nairobi nchini Kenya.

“Baraza hili ni muhimu katika kuhakikisha nchi za Afrika zinaungana kwa ajili ya kuendeleza rasilimali za umeme zilizopo pamoja na kupata umeme wa uhakika kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii, na katika Mkutano huu kila nchi imeonesha utayari kufanya biashara ya umeme pale kunapokuwa na umeme wa ziada.” Amesema Dkt. Biteko

Katika mkutano huo, Baraza la Mawaziri wanaohusika na mfumo wa pamoja wa umeme kwa nchi za Mashariki mwa Afrika  (EAPP Council of  Ministers-COM) limekubaliana kwa pamoja kuwa na usimamizi madhubuti wa miradi mbalimbali ya umeme katika nchi wanachama ili iweze kukamilika kwa wakati na kuwapatia wananchi nishati ya kutosha. #EastAfricaTV 

Kukamilika  kwa miradi kutoka vyanzo mbalimbali vya umeme, kutawezesha nchi hizo kusaidiana pale nchi mojawapo inapokuwa na upungufu wa umeme huku msisitizo ukiwekwa kwenye miradi ya usafirishaji umeme.(Transmission lines). 

Ameeleza kuwa  kuna idadi kubwa ya watu katika nchi wanachama wa EAPP, hivyo inahitajika nishati zaidi kwa ajili ya maendeleo ya watu na viwanda na ndio maana kila nchi imejikita katika kuendeleza vyanzo mbalimbali vya umeme ajili ya kujipatia nishati ya uhakika.

“Tanzania kuna njia mbalimbali za usafirishaji umeme (interconnectors) mfano Tanzania na Uganda, Tanzania na Burundi pamoja na Tanzania na Rwanda na sasa kuna laini ya umeme kutoka Tanzania hadi Kenya ambayo imekamilika na ipo kwenye majaribio itakayotuwezesha kufanya biashara kati ya nchi hizi mbili pale kila nchi ikiwa na umeme wa kutosha.”Amesema Dkt. Biteko

Ameongeza kuwa, kuna upembuzi yakinifu unafanyika chini ya  Benki ya Dunia (WB) kwa ajili ya kujenga mradi mkubwa wa usafirishaji umeme wa msongo wa Kilovoti 400 kutoka Tanzania hadi Uganda kutokea Shinyanga, ambao  utasafirisha umeme mwingi zaidi kwa baadhi ya mikoa kama vile Kagera na pia kuwezesha nchi hizo kufanya biashara ya umeme.

Awali, Mwenyekiti wa kikao hicho cha Baraza la Mawaziri wa Nishati ambaye ni Waziri wa Nishati na Petroli wa Kenya, Mhe. Davis Chirchir amesema lengo la nchi kuwa na mfumo huo  ni nchi wanachama 13 kufanya biashara ya mauziano ya umeme pale kunapokuwa na ziada ya umeme, na kwamba ili suala hilo liwezekane lazima kuwepo na miumbombinu ya umeme inayounganisha nchi hizo.

Amesema kuwa, majadiliano ya viongozi hao yamelenga katika kuimarisha muundo wa umoja huo pamoja na ushirikiano na hii ikijumuisha namna ya kukabiliana na changamoto mbalimbali za umeme pale zinapojitokeza. 

Viongozi wengine wanaoshiriki Mkutano huo kutoka Tanzania   ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Stephen Byabato, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mhandisi Gissima-Nyamohanga.