Jumatatu , 19th Feb , 2024

Wizara ya Afya imepokea taarifa inayosambaa mtandaoni ikiripoti kuwa Watu 7 wamepatwa na upofu kutokana na Ugonjwa wa Red Eyes.

Tunapenda kukanusha kuwa taarifa hiyo haijatolewa na Wizara ya Afya kama ilivyoripotiwa, taarifa hii inaweza kuleta taharuki zaidi ndani ya Jamii juu ya ugonjwa huu wa Macho Mekundu au kwa Kitaalam ‘Conjuctivitis’ (Red Eyes) 

Mnamo Februari 6, 2024, Mkurugenzi wa Huduma za Tiba kutoka Wizara ya Afya Prof. Paschal Ruggajo akizungumza na Waandishi wa Habari alinukuliwa akisema kuwa; Wizara imeanza kupokea taarifa za watu ambao wamefika kwenye vituo vya kutolea huduma za Afya wakiwa na vidonda kwenye kioo cha mbele cha jicho (Konea) walivyopata mara baada ya kutumia tiba zisizo rasmi kutibu ugonjwa wa ‘Red Eyes’  

Taarifa hiyo aliyoitoa haikutaja idadi ya watu waliopatwa na upofu kutokana ugonjwa wa Macho Mekundu kama ilivyotolewa kwenye Vyombo vya Habari. Prof. Ruggajo alitoa tahadhari kwa wananchi kuacha mara moja vitendo vya kujitibu kiholela ambavyo vinaweza kusababisha athari zaidi ikiwemo kupelekea upofu.  

Alisema kuwa baadhi ya watu wanatumia dawa zenye vichocheo vya Steriods, tangawizi, chai ya rangi iliyokolea majani, mafuta tete yaliyokuwa yanatumika wakati wa janga la UVIKO-19, maji ya chumvi huku wengine wakutumia mawiza ya mama njia ambazo sii sahihi na kuwasisitiza wananchi kufika kwenye vituo vya kutolea huduma za Afya ili kupata tiba sahihi za macho kutoka kwa wataalam. 

Wizara inavitaka vyombo vyahabari kuzingatia weledi wa taaluma ya habari kwa kutoa habari za ukweli kutoka kwenye vyanzo vilivyothibitishwa. Afya ni suala la msingi na linamgusa kila mmoja, taarifa zisizo za ukweli kuhusu huduma za Afya, magonjwa na Sekta ya Afya kwa ujumla zinaweza sababisha madhara zaidi kuliko hata lengo la utoaji wa taarifa wenyewe endapo taarifa haitokuwa sahihi. 

 Wizara ya Afya pamoja na Taasisi zake inawakaribisha waandishi wa habari kwa mikono miwili kufanya kazi kwa pamoja kwa kuzingatia maadili ya taaluma za pande zote mbili ili wananchi ambao ndio walengwa wa maudhui yanayotolewa na vyombo vya habari waweze kupata taarifa sahihi na zilizothibitishwa na wataalam au mamlaka husika.