Jumamosi , 30th Dec , 2023

Serikali ya Kenya imefunga kanisa la Maella, kaunti ndogo ya Naivasha, ambalo waumini wake hawatumii dawa za kawaida.

 

Kutokana na hali hiyo, imebainika kuwa baadhi ya waumini wa kanisa hilo wakiwemo watoto wadogo wamefariki dunia wakiwa majumbani mwao kutokana na magonjwa ambayo hayakufahamika.

Kufungwa kwa 'Kanitha wa Ngai' (Kanisa la Mungu), kunafuatia azimio la timu ya usalama ya kaunti ndogo ya Naivasha, baada ya vifo vya kutatanisha vya watoto wanne hivi majuzi.

Vifo hivyo vilizua taharuki kwa wananchi huku wakazi wakihoji shughuli za kanisa hilo linalopinga uganga wa kisasa.

Polisi na wakaazi hapo awali walikuwa wamewaokoa watoto wanne waliokuwa wagonjwa kutoka katika moja ya nyumba hizo na kuwakamata washukiwa wanne kwa madai ya uzembe.

Naibu Kamishna wa Naivasha Mutua Kisilu alisema polisi wanachunguza shughuli za 'dhehebu' hilo ambalo lina zaidi ya wanachama 200.