Jumatano , 22nd Nov , 2023

Katibu Mkuu wa CAM Daniel Chongolo amesema CCM itahakikisha serikali inaendelea kuweka mazingira bora na kuwajengea uwezo makandarasi na washauri waelekezi wazawa, ili waweze kutekeleza miradi mingi na mikubwa ndani ya nchi na hata kushindana nje ya Tanzania, ikiwemo kulipwa madeni yao

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Daniel Chongolo

na kuwahishiwa malipo ya kazi katika miradi wanayotekeleza.

Chongolo ameyasema hayo Novemba 21, 2023, wakati akitoa salam za chama kwenye mkutano wa Makandarasi na Washauri Waelekezi Wazawa, uliofanyika jijini Dodoma na amewaambia kuwa CCM inatambua changamoto zote zinazowasibu, likiwemo suala la madeni wanayodai na kucheleweshewa malipo yao katika miradi anuai wanayotekeleza maeneo mbalimbali nchini.

"Mkutano huu ni muhimu sana jana nimekaa na mawaziri wote wawili hawa, Waziri wa Ujenzi na Waziri wa Fedha hadi usiku wa manane, ilibidi tukae kwa muda mrefu sana, nilitaka kwanza kujua masuala kadhaa kabla sijaja hapa leo na hasa nililowaita na kuzungumza nao ni kuhusu malipo yenu, nina uhakika hapa tukisema tupitishe karatasi kila mtu aandike changamoto yake, jambo la kwanza kila mmoja litakuwa ni malipo, malipo, malipo," amesema Chongolo

Chongolo amesema hatua ya kuwatumia wakandarasi na washauri waelekezi wazalendo wa Kitanzania katika miradi hiyo mbalimbali ya ujenzi itaokoa fedha nyingi, ambazo kwa sasa zinalipwa kwa makandarasi wa nje, hivyo zitabakia katika mzunguko wa fedha na uchumi ndani ya nchi.

Aidha amewataka watendaji wa serikali, hususani katika Wizara ya Ujenzi kuacha mitazamo hasi dhidi ya wakandarasi na wahandisi wazawa kuwa hawawezi kazi, pia amewataka baadhi ya makandarasi wa ndani nao kuacha kuichafua tasnia ya ujenzi, kwa kuwa na kampuni za mfukoni (briefcase company), ambazo hazina uwezo wa kufanya kazi, hali ambayo inajenga na kuhalalisha dhana kuwa kuna wazawa wanafanya utapeli kwa kutumia taaluma hiyo.