Jumapili , 24th Sep , 2023

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.George Simbachawene, ametaka madaktari na walimu wasiwe wasimamizi wa miradi ya ujenzi inayotekelezwa katika maeneo yao ya kazi huku akisisitiza kuwa sio taaluma yao na ni matumizi mabaya ya rasilimali watu.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.George Simbachawene

Badala yake, ameutaka Uongozi wa Halmashauri zote nchini  hususan Halmashauri ya  Mpwapwa kuhakikisha inaachana utaratibu huo, iajiri wataalam wa fani ya ujenzi kwa ajili ya kusimamia miradi yote itakayokuwa ikitekelezwa katika Halmashauri hiyo ili iwe ya  viwango vya ubora kama ambavyo baadhi ya  Halmashauri zingine zinafanya.

"Kwa sasa majengo yetu yanajengwa na walimu na madaktari na badala ya kujengwa na  wahandisi wa ujenzi, hili halikubaliki hata kidogo," amesititiza Mhe.Simbachawene

Ameweka angalizo kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa imekuwa haifanyi vizuri katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya ujenzi kutokana na usimamizi hafifu kwa sababu  Wasimamizi wanaopewa jukumu hilo  sio taaluma yao. 

Amefafanua kuwa walimu au madaktari wanaosimamia miradi hiyo ujenzi sio kwamba ni wabadhirifu lakini kwa kuwa sio taaluma yao hivyo ni vigumu kuona na hata kushauri pale ujenzi unavyojengwa chini ya kiwango.

Amesema limekuwa ni jambo la kawaida kama mradi wa afya unatekelezwa basi msimamizi wa ujenzi atakuwa Daktari, vivyo hivyo kama ujenzi wa madarasa basi msimamizi atakuwa Mwalimu