Ijumaa , 8th Sep , 2023

Kundi la wanajeshi wa Sudan la Rapid Support Forces (RSF) limelaani vikwazo vya Marekani dhidi ya viongozi wake wawili, na kuvitaja vikwazo hivyo kuwa "visivyo vya haki na vya kushtua".

 

Siku ya Jumatano, Marekani ilimwekea vikwazo vya kifedha naibu kiongozi wa RSF Abdel Rahim Dagalo na marufuku ya kusafiri kwa kamanda wa kundi hilo katika jimbo la Darfur Magharibi, Jenerali Abdul Rahman Juma, kwa madai ya ukiukaji wa haki za binadamu.

Wote wawili Dagalo na Jenerali Juma wamekanusha madai hayo ya Marekani kama "uongo na upotoshaji".

Katika taarifa yake ya X (zamani Twitter) siku ya Alhamisi, RSF ilielezea vikwazo vya Marekani kama "kutisha, bahati mbaya na visivyo vya haki". Ilisema "haitasaidia kufikia moja ya malengo ya msingi ambayo yanapaswa kuzingatia, ambayo ni kutafuta suluhisho kamili la mgogoro katika nchi yetu".

Kundi hilo limeishutumu Marekani kwa kupuuza "uhalifu wa kutisha" uliofanywa na jeshi la kawaida la Sudan, ambalo limesema ni pamoja na mashambulizi ya mabomu ya kiholela katika maeneo ya raia na mateso ya wanaharakati wanaopinga vita.

Kundi hilo la kijeshi limesema vikwazo hivyo vitaathiri juhudi za Marekani za  kuleta amani ya kudumu nchini humo.