Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo Alhamisi Novemba 13, 2025 limemthibitisha Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu kuwa Waziri Mkuu mpya wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akiahidi kufanya kazi kwa bidii katika kuhakikisha kuwa maono na ahadi za Rais Samia Suluhu Hassan zinateketekelezwa ili kuwaletea wananchi ustawi na maendeleo kwa miaka mitano ijayo.
Uteuzi wa Mwigulu Nchemba aliyekuwa Waziri wa Fedha kwa miaka mitano ya awali ya serikali ya awamu ya sita, umetangazwa rasmi bungeni mjini Dodoma, akithibitishwa kwa kura 369 za ndio kati ya 371 zilizopigwa na wabunge huku kura mbili zikiharibika.
Akieleza kutambua namna ambavyo Dkt. Samia amejitambulisha kama Kiongozi wa matokeo, katika hotuba yake ya shukrani bungeni Dkt. Mwigulu ametoa rai kwa Watanzania kumtanguliza Mungu na kuhakikisha amani inaendelea kuwepo nchini, akitoa onyo kwa watumishi wazembe, wala rushwa na wenye lugha chafu kwa Watanzania.
"Kwa kuzingatia kazi kubwa iliyopo mbele yetu naomba niseme kuwa watumishi wa umma na Watanzania lazima tuwe tayari, lazima tuende na gia ya kupandia mlima, watumishi wa umma wavivu, wazembe, wala rushwa na wenye lugha mbaya kwa Watanzania tuwe tayari na nitakuja na fekeo na rato, lazima maono ya Rais na ahadi zake zitekelezwe." Amesisitiza Mhe. Mwigulu.
Aidha Mwigulu amemshukuru Rais Samia kwa imani yake kwake pamoja na Wabunge wenzake kwa kumuamini na kumkopesha imani, akisema Watanzania wote watasikilizwa kwa nidhamu kila ofisi ya umma na pamoja na kutoa nafasi sawa kwa wabunge wote wa Bunge la 13 hasa kwa wale walio wachache, wanaotokana na vyama vya upinzani.
Dkt. Mwigulu amewahi kushika nafasi mbalimbali serikalini. Alianza kama Naibu Waziri wa Fedha katika serikali ya awamu ya nne chini ya Rais Jakaya Kikwete. Baadaye aliteuliwa kuwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi mwaka 2015, kabla ya kuhamishiwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi mwaka 2016. Mwaka 2021 aliteuliwa kuwa Waziri wa Fedha, nafasi aliyoishikilia hadi uteuzi wake kuwa Waziri Mkuu.

