Alhamisi , 7th Sep , 2023

Viongozi wa kijeshi nchini Gabon wametangaza kumalizika kwa kifungo cha nyumbani cha rais Ali Bongo, wakisema kwa sasa yuko huru kuendelea na shughuli zake.

Mwaka 2018, Bw.Bongo alipatwa na kiharusi

Katika taarifa iliyosomwa kwenye televisheni ya taifa Jumatano jioni, msemaji wa jeshi Kanali Ulrich Manfoumbi alisema uamuzi wa kumuachia huru Bongo ulitokana na "hali yake ya kiafya".

Msemaji huyo aliongeza kuwa Bwana Bongo anaweza kusafiri nje ya nchi kama anataka kwa ajili ya uchunguzi wa kimatibabu.

Baada ya jeshi kufanya mapinduzi Agosti 30, walimweka rais huyo wa zamani katika kifungo cha nyumbani na kutangaza kuwa wanadhibiti taifa hilo lenye utajiri wa mafuta.

Uamuzi wa kumuachia huru unafuatia shinikizo kutoka kwa jumuiya ya kikanda ya Afrika ya Kati Eccas na majirani wa Gabon, kuheshimu uadilifu wa kimwili wa kiongozi huyo aliyeondolewa madarakani.

Mwaka 2018, Bw.Bongo alipatwa na kiharusi. Afya yake ilikuwa chanzo kikubwa cha wasiwasi kwa wengi katika kuelekea uchaguzi wa urais wa 2023.