
Azam FC imethibitisha uwepo wa mchezo huo kupitia kurasa zake za Mitandao ya Kijamii, baada ya Benchi la Ufundi kupendekeza kuchezwa kwa michezo hiyo angalau miwili katika kipindi hiki cha Kalenda ya FIFA.
Mchezo huo dhidi ya Gor Mahia umepangwa kuchezwa Jumamosi (Machi 26) katika Uwanja wa Nyayo jijini Nairobi nchini Kenya.
Kabla ya mchezo huo Azam FC itacheza mchezo mwingine wa kirafiki dhidi ya JKU kutoka visiwani Zanzibar Jumatano (Machi 22), katika Uwanja wa Azam Complex Chamazi jijini Dar es salaam.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Benchi la Ufundi Azam FC Dani Cadena amesema wamelazimika kukitumia kipindi hiki kwa mchezo huo, ili kuwaweka sawa wachezaji wao waliosalia kikosini, baada ya wenzao kumeitwa kuziwakilisha timu zao za taifa.
Mchezo wa mwisho kwa Azam FC ulikuwa ni Machi 13 ilipochapwa bao 1-0 na Ihefu FC kwenye Uwanja wa Highland Estate na baada ya hapo itacheza na Mtibwa Sugar katika Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ kati ya Aprili 1-6.