Alhamisi , 7th Sep , 2023

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kutokana na changamoto ya upatikanaji wa masoko ya bidhaa za kilimo nchini na nje ya nchi, serikali inaendelea na jitihada mbalimbali ili kupata soko la uhakika la bidhaa zote za kilimo.

Rais Dkt. Samia ameyasema hayo leo Septemba 07 alipokuwa akijibu mawali ya baadhi ya vijana waliopo kwenye mnyororo wa thamani wa kilimo waliotaka kujua ni kwa namna gani serikali inawasaidia wakulima katika suala la masoko ya bidhaa zao za kilimo hasa katika soko la nje ya nchi.

"Ni kweli suala la masoko bado kuna shida, lakini katika tafiti tulizozifanya tumegungua kuna mambo mawili yenye utata na tunayafanyia kazi, eneo la kwanza ni food balance sheet requirements (bidhaa gani inatakiwa wapi ndani na nje ya nchi) tukijua hili tutakuwa tunajua kitu gani tukizalisha kiende upande mwingine lakini ndani na nje" alisema Rais Dkt. Samia

Aidha Rais Dkt. Samia amesema katika eneo lingine utafiti wa serikali ulibaini bado katika eneo la connection ya mkulima na soko haijaifanya vizuri na wameanza kufanya kwenye baadhi ya mazao korosho ambapo tayari imeshuhudiwa mara kadhaa bei ya korosho ikipanda kwa sababu ya kuunganisha ushirika wa mkulima na mnunuaji moja kwa moja.

Zao jingine ambalo serikali haikufanya vizuri kwnye suala la soko ni katika kilimo cha Mbaazi ambapo Rais Dkt. Samia amesema baada ya kuhamasisha wakulima walime kwa wingi zao hilo mwisho wa siku lilikosa soko na wakulima walikata tamaa ya kuendelea kuzalisha lakini baada ya jitihada za serikali bei ya Mbaazi impenda kwa mwaka huu.

"Miaka miwili mitatu nyuma tulihamasisha wakulima walime Mbaazi na wakalima sana, lakini kwa sababu hatukuwaunganisha na soko na hatukuwa na mipango mizuri Mbaazi ilianguka sana bei na kuwavunja moyo wakulima, mwaka jana iliuzwa TZS. 300 kwa kilo lakini mwaka huu wakulima wameuza kwa TZS. 2000 kwa kilo, sasa huu ndiyo mtindo tutakaokwenda nao kwenye mazao mengine" alisisitiza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Kuhusu suala la usafiri unavyoweza kufungua masoko ya ndai na nje ya nchi, Rais Samia amesema serikali imejidhatiti kujenga barabara kunganisha mkoa na mkoa, wilaya na wilaya, mikoa na wilaya zake lakini pia ujenzi wa barabara kubwa na nchi jirani ili kuyafikia masoko ya nchi jirani. 

"Lakini siyo barabara peke yake tunatengeneza bandari zetu, Dar es salaam, Zanzibar, Tanga na Mtwara zote zipokee meli zinazoweza kuja kushusha na kuja kuchukua mazao mengine kwenda nje, na tumefanikiwa vizuri"

Akiwa amejikita kwenye usafiri Rais amesema serikali imenunua ndege ya mizigo ili iweze kusafirisha mazao hasa yale ya ambayo hayakai muda mrefu kuliko kutegemea usafiri kutoka kwa jirani apakie apeleke kwenye soko.

Rais Dkt. Samia amesema pia serikali inaendelea kutumia teknolojia katika kilimo kwakuwa ni jambo ambalo halikwepeki na linaondoa dhana ya kilimo ni kazi ngumu kwa kurahisisha shuguli za kilimo.

"Kwenye kilimo tumejielekeza kwanza kujua afya ya udongo kwahiyo kwa kutumia ICT tunaendelea kufanya usajili wa wakulima, aina ya kilimo wanachofanya, eneo wanalofanyia kilimo na mambo mengine yanayomuhusu mkulima" - Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan