Jumatano , 28th Jun , 2023

Chama cha Wanafunzi Madktari Tanzania (TAMSA) imeishukuru serikali kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya elimu nchini katika kada ya afya, ikiwa pamoja na kuendeleza ushirikiano mathubuti na mataifa jirani.

Akizungumza na waandishi wa habari katika hafla ya kuwakaribisha wanafunzi 150 wa mwaka wa tano waliotoka katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia ya Tiba nchini Sudan ambao wamehamishiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwaajili ya mafunzo ya vitendo, Rais wa Chama cha Wanafunzi Madaktari Tanzania (TAMSA)  Nehemiah Mtitu amesema kuwa hatua hiyo ni nzuri na italeta chachu katika kubadilishana uzoefu wa kitaaluma.

Aidha Mtitu amesema Chama cha Wanafunzi Madaktari wapo tayari kushirikiana nao katika shughuli za kitaaluma na kijamii kwa kipindi chote watakachokuwepo nchini ili kuchangia ustawi wa upatikanaji wa madaktari bora.

Wanafunzi hao 150 waliotoka katika Chuo kikuu cha Sayansi na Teknolojia ya Tiba nchini Sudan wapo nchini ili kupata mafunzo ya vitendo baada ya kufungwa kwa vyuo na shughuli mbalimbali za kijamii kusimama kutokana na mapigano yanayoendelea nchini humo.