
Ameshtakiwa kwa tuhuma za kupanga mapinduzi, madai ambayo anakanusha.
Jaji anayesimamia kesi ya Bolsonaro, Alexandre de Moraes, alisema uamuzi huo ni kwa sababu Bolsonaro hakufuata maagizo ya zuio aliyopewa mwezi uliopita.
Akijibu agizo hilo, timu ya wanasheria ya Bolsonaro ilikanusha kukiuka agizo lolote la zuio na kusema kwamba watakata rufaa dhidi ya uamuzi huo, kulingana na shirika la habari la Reuters.
Katika taarifa yake kwenye mtandao wa X, wizara ya mambo ya nje ya Marekani ilisema "inalaani" amri ya mahakama na "itawawajibisha wale wote wanaosaidia na kuunga mkono vikwazo vilivyoidhinishwa".
Donald Trump amesema kesi ya Bolsonaro ni "hila", huku akiitumia kuhalalisha ushuru wa 50% kwa baadhi ya bidhaa za Brazil licha ya Marekani kuwa na ziada ya biashara na nchi hiyo.
Bw Moraes, ambaye Marekani pia imemuwekea vikwazo, alisema Bolsonaro ametumia mitandao ya kijamii ya washirika wake wakiwemo wanawe kueneza jumbe zinazohimiza mashambulizi dhidi ya Mahakama ya Juu Zaidi na uingiliaji kati wa kigeni katika mahakama ya Brazil.