
Maadhimisho ya kuwaenzi mashujaa waliopigania haki na uhuru wa nchi dhidi ya utawala wa kikoloni yamefanyika katika leo Julai 25, 2025 viwanja vya Mashujaa vilivyopo makao makuu ya nchi, mjini Dodoma na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini na serikali.
Katika maadhimio hayo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye alikuwa ni mgeni rasmi, ameweka ngao na mkuki kama ishara ya kuwaenzi mashujaa hao.
Mwakilishi wa mashujaa waliopigana vita vya Kagera kati ya mwaka 1978 na 1979, Balozi Brigedia Jenerali Francis Benard Mndolwa mstaafu, ameweka shoka katika mnara wa kumbukumbu za mashujaa katika mji wa kiserikali, Mitumba, Dodoma ikiwa ni ishara ya kuwaenzi mashujaa hao.
Maadhimisho hayo maalum hufanyika kitaifa katika mkoa ambao huteuliwa kwa ajili ya shughuli hiyo na hupambwa na gwaride rasmi la mazishi ambalo hufuatiwa na uwekaji wa vifaa mbalimbali kama ngao, mkuki, shada la maua na sime katika minara ya kumbukumbu za mashujaa iliyojengwa sehemu mbalimbali nchini.
Miongoni mwa mashujaa waliolipigania taifa ni pamoja na baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Sheikh Abeid Aman Karume, Bibi Titi Mohammed, Abdulwahid Sykes pamoja na Rashidi Mfaume Kawawa, Waziri Mkuu wa pili wa Tanganyika na waziri mkuu wa kwanza wa Tanzania baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.