Jumamosi , 17th Jan , 2026

Msanii mshindi wa tuzo ya Grammy, Burna Boy, ameachia rasmi wimbo wake mpya “For Everybody” pamoja na filamu ya muziki, ikiwa ni mradi maalum aliouandaa kwa ushirikiano na Sporty Group.

Wasanii

Mradi huo wa kipekee unawakutanisha wanamichezo mashuhuri kutoka barani Afrika na nje ya Afrika , akiwemo Eduardo Camavinga, Nico na Iñaki Williams, Odion Ighalo, Claude Makelele, Christian Karembeu, Alex Song, Éder Militão, Asisat Oshoala, Cheslin Kolbe na wengineo. Kazi hiyo inaunganisha muziki, michezo na utambulisho wa Kiafrika, ikiwa ni maandalizi kuelekea mwaka muhimu kwa michezo ya Afrika.

Wimbo “For Everybody”, unaopatikana kupitia kurasa za YouTube za Burna Boy na SportyTV, unaendeleza dhamira ya msanii huyo ya kuhamasisha fahari ya Afrika, umoja na ushawishi wa bara hilo duniani. Wimbo huo ulizinduliwa siku chache kabla ya fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2026 kati ya Morocco na Senegal.

Mashabiki waliopata fursa ya kuhudhuria tamasha la AFCON Last Dance katika Ukanda wa Mashabiki wa Olm Souissi jijini Rabat, Ijumaa Januari 17, walishuhudia Burna Boy akiutumbuiza wimbo huo kwa mara ya kwanza moja kwa moja jukwaani.

Video ya muziki huo imeongozwa na muongozaji mashuhuri wa Marekani, Dave Meyers, kwa ushirikiano na dancer maarufu Shay Latukolan pamoja na Sporty Studios. Video hiyo inaonyesha kwa ubunifu mkubwa hisia, nguvu na ndoto zinazoendesha michezo ya Afrika, ikichanganya uigizaji wa wanamichezo, mitindo ya mavazi, dansi na simulizi za kitamaduni zinazotokana na soka na jamii.

Kupitia mashairi yanayozungumzia ustahimilivu, urithi na nguvu ya mshikamano wa pamoja, “For Everybody” ni heshima kwa kizazi kipya cha Waafrika wanaoacha alama zao duniani, ndani na nje ya viwanja vya michezo.

Akizungumzia wimbo huo, Burna Boy alisema:

“Huu ni wimbo kwa ajili ya utamaduni — kwa kila anayebeba sauti yetu, roho yetu na simulizi yetu duniani kote.”

Kwa upande wake, Dave Meyers alisema:

“Afrika ni bara lenye utajiri mkubwa wa kitamaduni, linalotambulika kwa uzuri, hadhi na utofauti usio na mipaka. Kualikwa kushiriki katika kusherehekea mitindo na harakati zake kupitia muziki wa Burna Boy ni heshima kubwa kwangu.”

Mradi huu unaashiria uzinduzi rasmi wa ulimwengu wa ubunifu ambao Burna Boy na Sporty Group wamekuwa wakiujenga kwa muda, baada ya video na matangazo ya awali yaliyoibua hamasa kubwa duniani.

Video ya muziki wa “For Everybody” sasa inapatikana kupitia chaneli ya YouTube ya Sporty Group.