Jumatatu , 19th Jun , 2023

Wanafunzi 150 wa udaktari kutoka Chuo Kikuu cha Tiba, Sayansi na Teknolojia (UMST) cha Khartoum nchini Sudan wamehamishiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ili kukamilisha mwaka wao wa mwisho wa masomo, kutokana na machafuko ya kisiasa nchini mwao yaliyosababisha vyuo kufungwa.

Wanafunzi wa Udaktari kutoka Sudan

Akiongea wakati wa kuwakaribisha wanafunzi hao, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Mohamed Janabi, amesema kuwa hali ya mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yanayoendelea nchini Sudani imesababisha kufungwa kwa vyuo na baadhi ya shughuli kusimama hivyo wataalamu hao kushindwa kuendelea na ratiba yao ya masomo ya kawaida.

"Wanafunzi hawa wapo mwaka wa tano wa shahada ya kwanza ya utabibu, ambapo katika mwaka huo, mafunzo hufanyika kwa vitendo zaidi, hivyo madaktari hawa wanafunzi watafanya mzunguko katika idara mbalimbali ikiwemo idara ya upasuaji chini ya usimamizi wa madaktari bingwa ili kuhakikisha wanapata maarifa yanayotakiwa," amesema Profesa Janabi

Amesema kuwa MNH itatoa fursa kwa wataalamu hao kujifunza kama ambavyo inatoa kwa wataalamu wengine wa ndani na nje ya nchi na hata baada ya kumaliza masomo kama watapenda kufanya mafunzo tarajali (Intenship) MNH itawapa nafasi hiyo.