
Boti mpya ya kisasa ya uokozi na matibabu (Modern Ambulance Boat) imezinduliwa kwa kushushwa majini na kufanyiwa majaribio kati ya jiji la Mwanza na kisiwa cha Ukerewe. Hatua hii ni sehemu ya maandalizi ya mwisho kabla ya kuanza rasmi kutoa huduma kwa wananchi wanaozunguka Ziwa Victoria.
Greyson Marwa, nahodha aliyeendesha boti hiyo wakati wa majaribio, amesema zoezi hilo limefanyika mara tu baada ya mkandarasi kumaliza kazi ya kuishusha kwenye maji katika Bandari ya Mwanza Kusini. Shirika la Usimamizi wa Usafirishaji Majini na Nchi Kavu (TASAC) lilifanya ukaguzi wa kina na kuendesha boti hiyo ili kujiridhisha kuwa ipo katika hali bora na tayari kwa kazi.
Boti hii ya uokozi na huduma za matibabu ni moja ya jitihada za serikali kupitia Wizara ya Uchukuzi kuhakikisha wananchi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa, hususan wavuvi na wakazi wa visiwa, wanapata huduma za haraka na za kuokoa maisha. Hii ni kutokana na ukweli kuwa shughuli kuu za kiuchumi katika eneo hili ni uvuvi, ambao mara nyingi huwahatarisha maisha wavuvi ndani ya Ziwa Victoria.
Kupitia boti hii, wananchi wanaoishi na kufanya shughuli zao katika maeneo ya Ziwa Victoria watanufaika na huduma za haraka za uokozi na matibabu pindi wanapopata dharura majini.