Jumamosi , 14th Feb , 2015

Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA kanda ya kaskazini kimeandaa mwongozo kwa ajili ya utendaji kazi wa viongozi wa serikali za mitaa waliochaguliwa hivi karibuni hatua inayolenga kuhakikisha kuwa wanawatumikia wananchi bila visingizio

Katibu wa chama hicho kanda ya kaskazini Bw Amani Golugwa amesema wanataka kuhakikisha kuwa ahadi za chama hicho kwa wananchi zinatumizwa kwa asilimia mia moja bila kuwepo kwa visingizio ili wananchi waweze kuona tofauti ya viongozi waliotoka chadema na wale wa CCM.

Kuhusu hatua iliyofikiwa katika kukabiliana na kero na malalamiko mbalimbali yakiwemo ya wa machinga Diwani wa kata ya daraja mbili Prosper Msofe ambaye pia ni Naibu Meya wa jiji amesema wanaendelea kuibana halmashauri na zinaendelea kufanyiwa kazi.

Kwa upande wao baadhi ya wamachinga wamesema hawana matumaiani ya kupatikana kwa ufumbuzi wa matatizo yao kwani utaratibu unaotumika kukabiliana na matatizo yaliyopo si shirikishi jambo linalosababisha mipango inayopangwa kuwa migumu kutekelezwa.

Wakati huo huo Mwenyekiti wa chama hicho taifa Freeman Mbowe amesema kuwa chama chao kimejipanga kuahakikisha kinahamasisha kwa nguvu zote wananchi weweze kwenda kujiandikisha katika daftari la mpiga kura

Mbowe amesema kuwa pamoja ya kuwa tume wamekuwa wanachelewesha kufanyika kwa zoezi hili, wao wamejipanga kikamilifu na pindi ambapo zoezi hili litatangazwa kuanza rasmi watajitahidi kwa njia yoyote kuhamasisha wananchi wajitokeze kwa wingi kujiandikisha

Kuhusu kupigia kura Katiba Inayopendekezwa Mbowe amesema wanaendelea na msimamo wao ambao waliutangaza awali wa kutoshiriki katika mchakato wa kura ya maoni ya katiba huku akisisitiza kuwa swala la kutoshiriki katika mchakato wa kura ya maoni hauingiliani kabisa na kuhamasisha wananchi kujiandikisha katika daftari la kudumu la mpiga kura