Jumanne , 6th Sep , 2022

Benki ya CRDB imezindua mashine mpya na ya kisasa ambayo itatumika na wateja wake kuweka fedha  (Cash deposite machine ) kwa lengo la kupunguza misongamano na foleni kwa wateja wao wanapokwenda kuweka fedha katika benki hiyo.

Mashine ya kuweka pesa taslimu

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Afisa Mkuu wa Uendeshaji wa benki hiyo Bruce Mwile, amesema huduma hiyo pia itawasaidia wateja wa benki hiyo ambao ni wafanyabiashara na wamekuwa wakifanya biashara zao mpaka nje ya muda wa kawaida kwenda kuweka fedha zao mara baada ya kufanya biashara zao.

Kwa upande wake Meneja wa CRDB Benki tawi la Mlimani City ambako ndio uzinduzi huo umefanyika Zaituni Manoro, amesema hapo awali hapakuwepo na mashine ya aina hiyo na tangu imewekwa imekuwa msaada mkubwa si kwa wafanyakazi pekee bali hata kwa wateja.

Nao baadhi ya wateja walioanza kuitumia mashine hiyo akiwemo Hassan Kafyome, mkazi wa changanyikeni Dar es Salaam amesema mashine hiyo imepunguza pia utaratibu wa awali ambao ulikuwa unamlazimu mteja anapotaka kuweka hela kuchukua karatasi za benki na kuandika kiasi unachotaka kuweka.