Jumatatu , 11th Jul , 2022

Mawakili wa upande wa utetezi katika kesi namba 10 inayomkabili Mfalme Zumaridi na wafuasi wake nane wameonesha kutokuwa na imani na Hakimu anayeendesha kesi hiyo na kuiomba Mahakama kutolea maamuzi ya sababu walizowakilisha ili ushahidi uendelee kutolewa.

Mfalme Zumaridi akiwa mahakamani

Mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Mwandamizi Monica Ndyekobora, wa Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Mwanza, Wakili wa upande wa serikali Emmanuel Luvinga, ameiambia Mahakama hiyo kuwa upelelezi wa kesi hiyo ya kujeruhi askari na kumzuia afisa ustawi kutekeleza majukumu yake umekamilika na kwamba mashahidi wawili ambao ni maaskari wa jeshi la polisi wapo tayari kutoa Ushahidi wao.

Baada ya Wakili wa serikali kuwasilisha hoja hiyo jopo la mawakili upande wa utetezi likiongozwa na wakili Stephen Kitale, wamesema mteja wao Zumaridi amesema hayupo tayari kuendelea na shauri hilo hadi maamuzi ya Mahakama yatolewe kutokana na sababu walizoziwakilisha kupitia mawakili hao.

"Mteja wetu ameonesha kutokuwa na imani na Hakimu anayeendesha shauri hili na kutokana na hilo tukashindwa kuendelea sababu utaratibu wa kisheria unatutaka pindi kunapokuwa na hoja kama hiyo ya kukosa imani kwa mheshimiwa au kama kuna sababu kama hiyo itapelekea mheshimiwa kujitoa kwenye shauri utaratibu uko wazi," ameeleza Wakili wa Zumaridi