Jumatatu , 18th Apr , 2022

Tanzania ni miongoni mwa nchi nne za Afrika zitakazonufaika na ufadhili wa Euro milioni 11 (sawa na Shilingi bilioni 30) kutoka Umoja wa Ulaya, ufadhili huo unaolenga sekta ya madini unatajwa kuongeza thamani katika sekta ya madini na biashara.

Wachimbaji wadogo wakiwa katika shughuli zao za kujiingizia kipato

Ufadhili huo umeelekezwa kwa Jumuiya ya Nchi za Afrika, Karibea na Pasifiki yaani (OACPS) yenye wanachama 79 ambapo kati yao ni wanachama wanne pekee waliochaguliwa. Uamuzi huo ulitangazwa na sekretarieti ya OACPS  yenye makao yake makuu mjini Brussels, Ubelgiji.

Mpango huo unaoitwa OACPS-EU Development Mineral Programme unalenga kuboresha mazingira ya uchimbaji madini na kuwawezesha wachimbaji wadogo, hasa vijana na wanawake katika sekta hiyo katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia 2022 hadi 2024. 

Aidha, tekelezaji wa mpango huu unatarajiwa kukuza sekta ya madini katika nchi za OACPS, na kutoa mchango mkubwa katika kuongeza mnyororo wa thamani wa madini, uzalishaji wa ajira na ukuaji wa uchumi, biashara na maendeleo kwa ujumla.

Hata hivyo, kuchaguliwa kwa Tanzania kunufaika na mpango huu kumetokana na kuimarika kwa ushawishi wa nchi ndani ya jumuiya ya OACPS na kazi nzuri inayofanywa na serikali chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha ushirikiano na jumuiya.