
Soko la kuku, Kawe
Wakizungumza na EATV leo Aprili 15, 2022 wafanyabiashara hao wamesema kuwa wateja wamekuwa wazito kununua kuku hasa kuku wa kisasa kwasababu wanatakiwa kukaangwa kwanza kabla ya kuliwa.
"Kwakweli Pasaka hii biashara ni ngumu, mimi ninauza kuku hawa wa kisasa. Ili walike ni lazima wakaangwe. Kwahiyo kinachotuumiza ni bei ya mafuta, mafuta ya kula lita hadi elfu 8. Mtu anashindwa kununua kuku na mafuta, inakuwa gharama kubwa bora anunue kitu kingine" -Mama Jack, muuza kuku Soko la Kawe.
"Kwakweli biashara ya kuku sasa hivi tofauti na miaka mingine, imekuwa ni ngumu. Hii inasababishwa na kupanda kwa bei ya mafuta ya kula, mteja anafikilia anunue kuku elfu 15 kisha atumie mafuta kumkaanga anaona ni bora anunue nyama buchani achemshe tu. Serikali ishushe bei ya mafuta ya kula"- Mama Kimaro, Mfanyabiashara wa Kuku, Kawe sokoni.
Kuhusu upatikanaji wa kitoweo hicho, wafanyabiashara hao wameiambia EATV kwamba kuku wapo wa kutosha sokoni japokuwa bei ya kuku imepanda kijijini kwa wafugaji ukilinganisha na misimu mingine ya sikukuu iliyopita. Wameongeza kuwa biashara imekuwa ngumu kwasababu ya kutokuwepo kwa wateja wa kutosha.
"Hali ya biashara ni ngumu Kwakweli, kuku wapo wa kutosha lakini wateja hakuna. Vilevile kijijini tunapowatoa kuku bei imepanda sana, ipo juu kwahiyo akipatikana mteja mmoja tunavutana"- Mbegu Abbas, Muuza Kuku Kawe Sokoni