
Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha kwa kushirikiana na maafisa kutoka tume ya kuthibiti dawa za kulevya wamefanya msako wa ghafla katika vijiji vya Kisimiri na Olkokola wilayani Arumeru na kufanikiwa kukamata na kuteketeza magunia 260 ya bangi huku watuhumiwa wakidaiwa kukimbia baada ya kuona askari hao.
Akizungumza akiwa katika eneo la operesheni hiyo iliyoanza majira ya saa Kumi Alfajiri afisa kutoka tume ya kudhibiti dawa za kulevya makao makuu January Ntisi amesema tume imeamua kuendeleza msako huo kwa kuwa takwimu zinaonesha kuwa idadi kubwa ya vijana wameathirika na dawa za kulevya ikiwemo bangi na hii inaweza kutengeneza taifa lenye kizazi chenye tabia mbaya na matendo ya uovu pamoja na kupunguza nguvu kazi ya taifa.
Kamanda wa jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha Liberatus Sabas amesema pamoja na kuonesha kuwa kilimo cha bangi kimeanza kupungua lakini bado wataendelea na msako na kuwataka viongozi wa vijiji na vitongoji kushirikana na jeshi katika kukomesha dawa hizo kwani wameonekana kuto toa ushirikiano huku akitoa angalizo kuwa jeshi halita mfumbia macho kiongozia atakaye bainika kujihusisha na kulimo cha bangi.
Baadhi ya wakazi wa maeneo hayo wamesema hata hivyo kiasi kilicho kamatwa ni kidogo kwakuwa watu wamekuwa wajanja kwani mwaka huu wameuza mapema kwakuwa wameshajua miezi inayofanywa msako na kuliomba jeshi la Polisi libadilishe mbinu za msako wake.