
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga.
Waziri Hasunga ametoa agizo hilo wakati akizungumza na wananchi mara baada ya kutembelea skimu ya umwagiliaji ya Kitere iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara.
Amesema kuwa gharama za uchimbaji wa kisima kimoja kwa ajili ya umwagiliaji haipaswi kuzidi shilingi Milioni 20 kwani kufanya hivyo ni kinyume na utaratibu na kushindwa kuakisi kasi ya utendaji wa Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe Rais Dkt John Pombe Magufuli.
Katika ziara hiyo Waziri Hasunga ameiagiza Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kuchimba visima vitatu katika eneo hilo kwa kiasi cha shilingi milioni 60 ikiwa ni shilingi milioni 20 kwa kila kisima kimoja.
Amesema kuwa umefika wakati wa wakulima kuachana na kilimo cha kutegemea mvua za msimu badala yake kuhakikisha kuwa wanalima kilimo bora cha umwagiliaji.
Kadhalika amekumbushia agizo lake alilolitoa hivi karibuni la kila mkoa kuwa na Afisa umwagiliaji wa mkoa huku wilaya zote zenye skimu za umwagiliaji kuwa na afisa umwagiliaji wa wilaya.
Waziri Hasunga amesema kuwa mkakati huo madhubuti wa serikali kuhakikisha kunakuwa na skimu nyingi za umwagiliaji utaimarisha sekta ya kilimo jambo litakaloongeza kipato cha mtu mmoja mmoja sambamba na Taifa kwa ujumla wake.