Alhamisi , 1st Nov , 2018

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeelezwa kuwa Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe ameshindwa kufika mahakamani kwa kuwa amepelekwa nje ya nchi kwa ajili ya matibabu, ambapo inadaiwa Mbowe anasumbuliwa na ugonjwa wa moyo na shinikizo la damu.

Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe

Kauli hiyo imetolewa mahakamani leo Novemba 1 na mdhamini wa Mbowe, Grayson Celestine aliyedai kuwa amepewa taarifa za ugonjwa wa Mbowe na mke wa mwanasiasa huyo.

"Kwa mujibu wa maelezo ya mkewe, Mbowe anasumbuliwa na matatizo ya moyo pamoja na shinikizo la damu na familia imeamua kumsafirisha afrika kusini kwa dharura lakini mimi sijaonana naye" amesema Celestine.

Aidha Celestine alimueleza Hakimu Mashauri kuwa “mshtakiwa Freeman Mbowe akirejea atawasilisha nyaraka za safari na matibabu, kwamba anaendelea kufanya mawasiliano ili azitume nyaraka kwa njia ya mtandao.”

Kufuatia maelezo hayo, wakili wa Faraja Nchimbi aliomba kutolewa kwa amri ya kumkamata Mbowe ili ajieleze sababu za kutofika mahakamani.

Sisi upande wa mashtaka hiyo tunaona ni mwendelezo wa dharau ya mshtakiwa Mbowe kwa mahakama kwa kuwa alishapewa onyo, Mbowe ameamua kwa utashi wake kukiuka amri ya mahakama”, amesema Faraja Nchimbi.

Kiongozi huyo wa CHADEMA na viongozi wengine wanatuhumiwa kwa makosa mbalimbali ikiwemo kuratibu na kufanya maandamano yaliyosababisha kifo cha aliyekuwa mwanafunzi Chuo cha Taifa  Usafirishaji NIT, Akwilina Akwilini.