Alhamisi , 1st Mei , 2025

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kimeshtushwa na taarifa za kushambuliwa kwa Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Dk Charles Kitima.

Kushoto ni Katibu Mkuu wa CCM Balozi Dkt Emmanuel Nchimbi, na kulia ni Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Dk Charles Kitima.

Kupitia taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa chama hicho Balozi Dkt Emmanuel Nchimbi, CCM imetoa wito kwa vyombo vya usalama kufanya uchunguzi wa kina na haraka ili kuwabaini na kuwachukulia hatua kali wahusika wa tukio hilo.

"CCM inatoa pole kwa Padre Dkt. Charles Kitima, familia yake, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, na waumini wote wa Kanisa Katoliki kwa mshtuko na maumivu yaliyosababishwa na tukio hili. Tunamuombea uponaji wa haraka na kurejea katika majukumu yake ya kiroho na kijamii. CCM itaendelea kushirikiana na taasisi zote za dini katika kujenga taifa lenye kulinda na kuendeleza misingi ya amani, umoja wa kitaifa, mshikamano, heshima na linaloheshimu haki za binadamu," imeeleza taarifa hiyo

Dk Kitima ambaye anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Aga Khan ameshambuliwa jana usiku Aprili 30, 2025 Kurasini Dar es Salaam, zilipo ofisi za Makao Makuu ya Baraza la Maaskofu Tanzania.