Jumatatu , 28th Apr , 2025

Utafiti mpya umeonesha kuwa matumizi ya nguvu za kijeshi duniani yameongezeka huku Migogoro ikitajwa kuchochea hali hiyo

Ripoti mpya iliyotolewa na Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa masuala ya Amani (SIPRI) imesema matumizi ya kijeshi duniani kote yameongezeka mwaka jana huku migogoro inayoongezeka ikichochea ongezeko la matumizi hayo.

Ripoti hiyo ya taasisi ya SIPRI yenye makao yake katika mji mkuu wa Sweden Stockholm iliyotolewa leo Jumatatu imesema matumizi ya kijeshi yameongezeka kote duniani kwa kasi zaidi tangu kumalizika kwa Vita Baridi na kufikia dola trilioni 2.7, huku ikisisitiza kuwa ongezeko kubwa la matumizi ya kijeshi limeshuhudiwa zaidi barani Ulaya na Mashariki ya Kati.

Ripoti hiyo imesema  mataifa yote ya Ulaya kasoro Malta yameongeza maradufu matumizi yao ya kijeshi huku Marekani ikisalia kileleni ambapo matumizi yake ya kijeshi yalifikia dola bilioni 997. 

Wakati vita nchini Ukraine vikiingia katika mwaka wake wa tatu, matumizi ya kijeshi yameendelea kuongezeka kote barani Ulaya, hadi kufikia asilimia 17 ambayo ni sawa na dola bilioni 693.

Mwaka 2024, Urusi iliongeza matumizi yake ya kijeshi hadi kufikia dola bilioni 149, Ukraine bilioni 64.7, Ujerumani iliongeza matumizi yake ya kijeshi kwa asilimia 28 hadi kufikia dola bilioni 88.5 bilioni, na kuiweka katika nafasi ya nne duniani. Mataifa mengine kama Israel yametajwa pia kuongeza matumizi yao ya kijeshi.

Ripoti hiyo ya taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa masuala ya Amani (SIPRI) imeongeza kuwa matumizi hayo yaliongezeka kwa asilimia 9.4 kote duniani ikilinganishwa na mwaka 2023, huku 2024 ikiorodheshwa kuwa mwaka wa 10 mfululizo wa ongezeko la matumizi ya kijeshi ulimwenguni. 

Nchi tano ndizo zimetajwa kutumia fedha nyingi zaidi kwa matumizi ya kijeshi nazo ni Marekani,China, Urusi, Ujerumani na India ambazo zinachangia kwa asilimia 60 ya matumizi jumla ya kijeshi kote duniani.