Jumanne , 29th Apr , 2025

Wakati uchaguzi wa Papa mpya ukiendelea kusubiriwa kwa hamu duniani, Kadinali aliyehukumiwa kwa ubadhirifu wa fedha ametangaza kujiondoa katika uchaguzi huo

Giovanni Angelo Becciu, ambaye aliwahi kuwa miongoni mwa viongozi wenye ushawishi mkubwa ndani ya Vatican, amesema hatashiriki katika mkutano wa siri wa kumchagua Papa mpya, baada ya kuhukumiwa kwa makosa ya kifedha.

Mnamo mwaka 2020, Papa Francis alimuamuru Kadinali Becciu kujiuzulu hadhi na haki zote za ukadinali kufuatia kuhusishwa kwake na sakata la kifedha ndani ya Vatican.

Baada ya kifo cha Papa wiki iliyopita, Kadinali Becciu alikata rufaa akitaka kurejeshewa haki ya kushiriki katika mkutano huo muhimu.

Hata hivyo, tarehe 29 mwezi Aprili ametoa taarifa rasmi akitangaza kujiondoa.
Kwa mujibu wa taarifa ya Vatican iliyotolewa Jumatatu, makadinali wamepanga kuanza mkutano huo wa siri tarehe 7 Mei, kwa ajili ya kumchagua kiongozi mpya wa Kanisa Katoliki, linalowakilisha waumini takribani bilioni 1.4 duniani kote.

Uamuzi wa Becciu kujiondoa umetolewa siku saba tu baada ya kuliambia gazeti moja la Sardinia kuwa hakukuwa na tamko la wazi la kumuondoa katika mkutano huo, wala agizo la maandishi linalomtaka ajiondoe rasmi.
Becciu alipatikana na hatia ya ubadhirifu na ulaghai mwaka wa 2023 na akahukumiwa kifungo cha miaka mitano na nusu jela.

Yeye ndiye kadinali wa kwanza kuhukumiwa na mahakama ya jinai ya Vatican na Anaruhusiwa kuendelea kuishi katika ghorofa ya Vatikani wakati mchakato huo ukiendelea.